Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya wanafunzi wa shule ya msingi nchini Iran ni jambo la kushangaza.

Maria Zakharova ameashiria shambulizi la Marekani na Israel lililolenga shule ya msingi ya wasichana ya Shajara Tayyibah kusini magharibi mwa Iran na kusema: Kimya cha vyombo vya habari vya kimataifa mbele ya mauaji ya wasichana wa shule ya msingi nchini Iran kinashangaza sana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, hakuna hata mmoja kati ya waliotekeleza uhalifu huo au waliouunga mkono ambaye ameeleza kusitikishwa na tukio hilo, kutoa mkono wa pole au hata kulitambua kuwa ni jinai. 

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Jumamosi iliyopita shambulizi la Marekani liliua shahidi wasichana 165 waliokuwa na umri wa kati ya miaka 7 na 12 wakiwa madarasani katika Shule ya Msingi ya Minab nchini Iran na karibu walimu wao 20. Mazishi ya wanafunzi hao wa kike wa shule ya msingi huko kusini mwa Iran, yalifanyika jana kwa huzuni kubwa na majonzi, huku wazazi waliokuwa wakiomboleza wapendwa wao wakitoa wito wa kulipiza kisasi dhidi ya mauaji hayo.

George Galloway, mbunge wa zamani wa Uingereza amesema mauaji hayo ya halaiki yaliyofanywa na Marekani dhidi ya wanafunzi wa kike 165 nchini Iran ndio maafa makubwa zaidi yaliyowahi kufanywa na Marekani tangu wakati wa Vita vya Vietnam.

Wakati huo huo, Waziri wa Elimu Iran, Alireza Kazemi, amesema hadi sasa wanafunzi wasiopungua 185 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, Jumamosi iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *