
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto imetoa wito leo Jumatano kwa watoto kulindwa wakati wa vita Mashariki ya Kati, ikirejelea hasa tukio la shambulio dhidi ya shule moja ya wasishana nchini Iran siku ya Jumamosi, Februari 28.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa, kamati hiyo, iliyojumuisha wataalamu 18 huru, imesema “ina wasiwasi mkubwa na vurugu zinazoongezeka Mashariki ya Kati na athari zake kubwa kwa watoto.” Kamati hiyo “imeshtushwa na ripoti za mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia, ikiwa ni pamoja na shule na hospitali, ambayo yamejeruhi na kuwatia kiwewe watoto na kuwaua vijana wengi.”
Taarifa hiyo inataja haswa tukio la shambulio dhidi ya shule ya wasichana katika mji wa Minab nchini Iran. Mamlaka ya Iran ilitangaza vifo 150 katika shambulio hili linalodaiwa siku ya kwanza ya vita.
Sio Marekani wala Israel imethibitisha shambulio hilo, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwamba Pentagon inafanya uchunguzi. Shirka la habari la AFP halikuweza kufikia eneo la tukio ili kuthibitisha kwa uhuru takwimu za majeruhi au mazingira ya tukio hilo.
“Hii inatukumbusha kwamba watoto ni miongoni mwa walio hatarini zaidi katika migogoro ya kivita na hawapaswi kamwe kuchukuliwa kuwa wahusika katika vita,” kamati ya Umoja wa Mataifa imesema, kabla ya kubainisha kwamba “watoto lazima walindwe kutokana na athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za uhasama. Pande zote (…) zinawajibika kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”
Kwa hivyo, kamati inazitaka pande hizo kuchukua hatua zinazohitajika kuwalinda watoto, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shule, hospitali, na miundombinu mingine ya kiraia haishambuliwi, na kwamba watendaji wa kibinadamu wanaweza kuwafikia kwa usalama watoto na familia zinazohitaji msaada.