
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmail Baghaei amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haizishambulii nchi jirani, bali inavilenga vituo vya kijeshi na vya maslahi ya Marekani vilivyoko katika eneo hili.
Baghaei ametoa ufafanuzi huo katika mahojiano na chaneli ya Al-Arabiyya na kukumbusha kuwa, Iran imeandamwa na mashambulizi yasiyo na uhalali wa kisheria ya Marekani na utawala wa kizayuni.
Amesema, harakati za Iran zinazoshuhudiwa hivi sasa katika eneo zinafanyika kwa msingi wa “kujihami” na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haina uadui wowote na majirani zake wala nia yoyote ya kuzishambulia nchi hizo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amesisitiza kuwa, katika mashambulizi yake, vikosi vya majeshi ya Iran vinavilenga, tena kwa umakini, vituo vya Marekani tu; na kwamba kinachojiri hivi sasa ni Iran kujihami kulingana na kifungu cha 51 cha sheria za kimataifa.
Katika mahojiano hayo na Al-Arabiyya, Baghaei ameendelea kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishambuliwa kijeshi kinyume na sheria na Marekani ikishirikiana na utawala wa kizayuni katika siku ya 10 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwamba huo ndio uhakika wa mambo.
Amesema: “hiyo ilikuwa jinai kubwa na uchokozi wa wazi dhidi ya uhuru na mamlaka ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na sisi tulishatangaza tokea kabla kwamba, ikiwa tutaandamwa na shambulio lolote, tutatoa jibu kali na la kila mahali”.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ameongezea kwa kusema: “ninasisitiza kwamba, Iran inazinyooshea mkono wa urafiki nchi zote jirani za eneo na nchi zote za Kiislamu”…/