Nigeria. Vizuri havidumu ni kauli ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara pale ambapo jamii inapopoteza mtu muhimu, awe ni mzazi, kiongozi, mfanyabiashara au msanii anayependwa na wengi. Ni maneno yanayobeba majonzi, mshangao na maswali yasiyokuwa na majibu.
Ndivyo ilivyokuwa kwa kifo cha Ilerioluwa Oladimeji Aloba maarufu Mohbad, nyota chipukizi wa muziki wa Nigeria aliyeng’ara kwa muda mfupi lakini akaacha alama kubwa. Alikuwa sauti ya vijana wa mitaani, alama ya kizazi kipya cha Afrobeat na sura ya matumaini kwa wengi waliotamani kuona ndoto zao zikitimia kupitia muziki.
Lakini kama ilivyo kwa simulizi nyingi za mastaa wanaopanda kwa kasi, safari yake haikukosa misukosuko. Kulikuwa na tuhuma, migogoro ya kazi, presha za tasnia na hatimaye kifo chake kilichozua taharuki kubwa nchini Nigeria na nje ya mipaka yake.
Hii ni simulizi ya maisha yake, kutoka kupambania mitaani hadi kuwa gumzo Nigeria, na jinsi kifo chake kilivyogeuka mjadala mpana wa haki, uwajibikaji na mustakabali wa wasanii chipukizi.
Mwananchi linakujuza kuanzia mwanzo wa safari ya muziki, misukosuko aliyokumbana nayo hadi umauti kumfika, ikiwa inakaribia miaka minne sasa tangu afariki na hadi sasa hajazikwa.
SAFARI YAKE
Mohbad, jina lake halisi Ilerioluwa Oladimeji Aloba, alizaliwa mwaka 1996 huko Lagos, Nigeria. Alijipambanua kupitia nyimbo zenye mdundo wa haraka, mashairi ya maisha ya mtaani na sauti ya kipekee iliyogusa vijana wengi.
Maisha ya muziki alianza mwanzoni mwa mwaka 2019 akiimba mitaani na akaanza kukubalika miongoni mwa vijana.
Alipata umaarufu mkubwa baada ya kusainiwa na lebo ya Marlian Records inayomilikiwa na msanii maarufu Naira Marley. Kupitia lebo hiyo alitoa nyimbo zilizopokelewa vizuri kama ‘Ponmo’, ‘Feel Good’ na ‘KPK (Ko Por Ke)’ aliomshirikisha Rexxie.
Mohbad aliachia albamu yake ya kwanza iliyoitwa ‘Light’ mwaka 2020, ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya wimbo wake ‘Ponmo’ aliomshirikisha Naira Marley pamoja na Lil Kesh kufanya vizuri zaidi.
Kupitia albamu hiyo, Mohbad alizidi kujiongezea umaarufu katika tasnia ya muziki wa Nigeria, akionesha uwezo wake wa kuunganisha mitindo ya Afrobeat na sauti ya mtaani iliyomtofautisha na wasanii wengine.
Kutokana na kazi zake, alichaguliwa mara tano kuwania tuzo za The Beatz Awards za mwaka 2021, jambo lililoonesha namna alivyopambania kazi yake.
Ndani ya muda huo, Mohbad alikibadilisha kizazi cha Marlian, akionekana kuwa mrithi wa mtindo wa muziki wa mtaani uliochochewa na Naira Marley. Lakini nyuma ya pazia, mambo hayakuwa shwari.
Misukosuko ya kazi
Mwaka 2022 alitangaza hadharani kuondoka kwenye lebo hiyo kufuatia matukio ya kunyanyaswa, kufanyiwa vurugu na baadhi ya watu kwenye lebo hiyo.
Video zilizosambaa mitandaoni zilimuonyesha akidai kupigwa na kutishiwa. Katika moja ya malalamiko yake, alisema maisha yake yako hatarini na akawataja baadhi ya watu waliokuwa wakimpa presha.
Baadaye, Mohbad akaondoka rasmi Marlian Records. Mgogoro huo uliibua mjadala mkubwa Nigeria kuhusu haki za wasanii, mikataba inayowakandamiza na nguvu za lebo dhidi ya vipaji chipukizi.
Baada ya kuondoka, alijaribu kujitengeneza upya kama msanii huru. Mashabiki waliamini sasa yuko huru na mafanikio makubwa zaidi yanakuja.
Utata wa kifo chake
Septemba 12, 2023, taarifa za kifo cha Mohbad zilisambaa zikidai kuwa amefariki dunia. Taarifa za awali zilieleza kuwa alifariki baada ya kupatiwa matibabu kufuatia maumivu ya sikio na kupigwa sindano.
Hata hivyo, mazingira ya kifo chake yalizua taharuki kubwa nchini humo. Mashabiki walijaa mitaani wakitaka haki, wakiamini huenda kulikuwa na mkono wa mtu nyuma ya kifo cha supastaa wao.
Kelele za wananchi zilisababisha Jeshi la Polisi la Nigeria kuanzisha uchunguzi rasmi. Mwili wa Mohbad ulifukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake.
Watu kadhaa waliitwa kuhojiwa, wakiwemo waliokuwa karibu naye kikazi na kifamilia. Uchunguzi huo uliendelea kwa miezi kadhaa huku mamlaka zikiahidi kutoa ukweli kwa umma.
Ripoti za awali za kitabibu zilionesha kuwa chanzo kamili cha kifo hakikuweza kuwekwa wazi kutokana na hali ya mwili, jambo lililoongeza sintofahamu zaidi.
Licha ya safari yake kukatizwa ghafla, Mohbad ameacha alama kubwa katika muziki wa Nigeria. Nyimbo zake ziliendelea kufanya vizuri na kushika nafasi za juu kwenye chati za muziki baada ya kifo chake, zikionesha namna alivyogusa mioyo ya watu.
Nje ya hapo pia ameacha alama kubwa kwa mashabiki ambao kwa namna hiyo inaonyesha alikuwa anaigusa jamii kupitia mashairi yake yenye nguvu ya kukemea uovu na unyonyaji.
Mashabiki wake walifanya kampeni ya ‘Justice for Mohbad’ wakitaka ukweli ujulikane na yeyote atakayebainika kuwajibika achukuliwe hatua.
Familia yake
Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa familia yake haikuwa mstari wa mbele kupambania haki ya kijana huyo, baadhi wakisema ni kama kutozikwa kwake kuna faida kwa familia hiyo.
Ripoti hizo zinaeleza kuwa wakati kesi hiyo inashughulikiwa na Serikali ya Nigeria, wazazi na ndugu wa Mohbad bado wanaendelea kupewa michango ya msiba.
Inaelezwa pia kuwa mtoto wake wa kiume aitwaye Liam, familia inataka kujiridhisha kwa kufanya vipimo vya DNA kujua kama kijana huyo ni damu yao halali au la.
Hata hivyo, kwa sasa mke wa Mohbad na mtoto wake wanaishi na kuhudumiwa na mama mkwe wa msanii wa Tanzania, Juma Jux, muigizaji Iyabo Ojo.