
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), mnamo Machi 2, 2026, lilitangaza kuwa wamepoteza mawasiliano na wafanyakazi wake 26 katika Jimbo la Jonglei, nchini Sudan Kusini, ambapo mapigano kati ya makundi hasimu yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Siku mbili baadaye, shirika hilo lisilo la kiserikali badohalina taarifa yoyote kuhusu wafanyakazi wake, ambao “wametawanyika porini,” anaelezea Marietta Nagtzaam, Naibu Mkuu wa MSF nchini Sudan Kusini. “Hadi tutakapowasiliana nao, hatuwezi kuthibitisha ikiwa wako salama au la,” anasema.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) lina wasiwasi kuhusu mgogoro mbaya wa kibinadamu na afya nchini Sudan Kusini. Mgogoro nchini Sudan Kusini umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni, hasa katika Jimbo la Jonglei (mashariki-katikati), ambapo jeshi la serikali limekuwa likishambulia maeneo yanayodhibitiwa na wafuasi wa Riek Machar, makamu wa rais aliyeondolewa mamlakani ambaye anazuiliwa kwa karibu mwaka mmoja sasa. Angalau watu 280,000 wametoroa makazi yao katika maeneo haya, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Hospitali ya MSF katika mji wa Lankien pia ilikumbwa na mashambulizi ya mabomu. Shirika hili lisilo la kiserikali linaripoti kupoteza mawasiliano na wafanyakazi wake 26 katika jimbo hilo kutokana na vurugu hizo, anaelezea Marietta Nagtzaam, naibu mkuu wa MSF nchini Sudan Kusini. “Bado tuna wafanyakazi wetu, lakini tatizo ni kwamba, kutokana na ongezeko la vurugu hivi karibuni, wamekimbilia msituni,” amemwambia mwandishi wetu Alexandra Brangeon. “Hivi sasa, bado tuna wafanyakazi 26 ambao tumepoteza mawasiliano nao.” Wametawanyika kote msituni, wakielekea kaskazini na mashariki, wakitafuta usalama. Hatujui kama ni kwa sababu tu wako mahali fulani na wamekosa mtandao ili kuweza kuwasiliana nasi, lakini hadi tutakapowasiliana nao, hatuwezi kuthibitisha kama kweli wako salama au la”.
“Mashahidi wanasema vituo vyote vya afya vimechomwa moto”
Marietta Nagtzaam anaendelea: “Tulikuwa na vituo vya afya vinavyosaidiwa na MSF huko Lankien na Pieri katika Jimbo la Jonglei. Kulikuwa na vurugu nyingi, na bado hatujaweza kurudi. Lakini kuna mashahidi wanaosema vituo vyote vya afya vimechomwa moto. Kwa hivyo, kwa sasa, huduma za matibabu hazipatikani tena huko. Watu wote wamekimbia pande tofauti.” Kwa hivyo, katika maeneo mengine, tunapeleka shughuli na timu zetu kutoa majibu ya dharura, pamoja na kliniki zinazohamishika.”
Jonglei ni eneo linalokabiliwa na mapigano makubwa kati ya jeshi linalomtii Rais Salva Kiir na wanamgambo wanaomuunga mkono mpinzani wake wa muda mrefu Riek Machar, ambaye yuko chini ya kifungo cha nyumbani kwa karibu mwaka mmoja na anashtakiwa kwa “uhalifu dhidi ya ubinadamu.”
Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani, imekuwa ikikumbwa na vita na ufisadi ulioenea tangu uhuru wake kutoka Sudan mwaka wa 2011.
Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulionya kuhusu hatari ya kurudi kwenye “vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoenea.” Mzozo wa umwagaji damu kati ya wafuasi wa Salva Kiir na Riek Machar ulisababisha vifo vya watu wapatao 400,000 na watu milioni nne waliokimbia makazi yao kati ya mwaka 2013 na 2018.