Kituo cha Afya cha Rufaa cha Rubaya, kilichopo takriban kilomita 70 kutoka mji wa Goma, katika Ukanda wa Afya wa Vijijini wa Kirotshe katika jimbo la Kivu Kaskazini lililoathiriwa na migogoro.

Jonas Imany, Muuguzi Msimamizi, Ukanda wa Afya wa Kirotshe anasimulia akiwa kwenye jimbo la kirotshe; anasema, “tupo hapa katika Kituo cha Afya cha Rufaa cha Rubaya. Tumefuatana na mshirika wetu, Shirika la Afya Duniani (WHO), ambao wamewasilisha dawa kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa katika kituo hiki cha rufaa cha Rubaya. Tumeridhishwa sana na msaada huu kutoka WHO kwa sababu unajibu mahitaji yaliyotolewa na vituo vya afya. Hivi punde tumepokea dawa za kuwahudumia watu wanaougua magonjwa kama vile kipindupindu.”

Mji wa Rubaya umekumbwa na matukio kadhaa, ikiwemo maporomoko ya ardhi ya hivi karibuni pamoja na milipuko ya magonjwa ya kipindupindu, surua na mpox. Kupitia ofisi yake iliyoko Goma, WHO ilitoa karibu tani sita za dawa na vifaa kwa ajili ya huduma za dharura na matibabu ya majeraha, pamoja na matibabu ya magonjwa ya kipindupindu, surua na mpox.Aidha, WHO ilitoa vifaa vya kuzuia na kudhibiti maambukizi katika vituo vya huduma za afya.

 Anitha Izabiriza, Muuguzi Aliyesajiliwa wa Kituo cha Afya cha Rubaya akisimulia jinsi masaibu yanayo wakumba anasema, “tumeona watu wengi waliokimbia makazi yao wakitoka Katoyi, kwa sababu mapigano bado yanaendelea upande wa pili. Kutokana na hali hii, hatukuwa na dawa za kutosha, na ikawa vigumu kupokea watu zaidi waliokimbia makazi yao na kuwapatia huduma za afya, kwa kuwa hawakuwa na fedha za kulipia matibabu.”

Dkt. Didier Mwesha, Mkuu wa Operesheni za Afya na Utaalamu wa Kiufundi, WHO anaeleza zaidi akisema, “eneo la afya la Rubaya linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo maporomoko ya ardhi ya hivi karibuni yaliyolathiri eneo hilo pamoja na milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, kifua kikuu na surua. Kupitia ofisi yake ndogo ya Goma, Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuja kusaidia wananchi wanaokumbwa na changamoto hizi mbalimbali kwa kutoa karibu tani sita za dawa, zikiwemo vifaa vya matibabu ya majeraha ya dharura pamoja na dawa za kutibu surua na kipindupindu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *