Siku saba tangu mabomu ya Israel na Marekani nchini Iran yalipochochea mashambulizi ya kulipiza kisasi katika Mashariki ya Kati, Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu yamethibitisha athari za mgogoro huo katika ukanda wakitoa mifano ya maeneo mbalimbali.

Raia wametwama kwenye mateso na huzuni – OHCHR

Ravina Shamdasani, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) amesema, “uvamizi wa ardhini wa jeshi la Israel kusini mwa Lebanon, amri za kuwahamisha watu kwa wingi katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, eneo la Bekaa na maeneo yote kusini mwa Mto Litani, pamoja na mashambulizi ya anga yanayoendelea katika sehemu mbalimbali za nchi, vinaongeza mateso na huzuni kwa raia ambao tayari wamechoka.”

Bi. Shamdasani, pia ameangazia hali ya watu nchini Afghanistan, ambako inaripotiwa kuwa watu 66,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano ya hivi karibuni na Pakistan.

“Nchini Pakistan pia, mashambulizi ya mizinga na silaha nyingine yamelazimisha watu kukimbia makazi yao, na raia katika pande zote za mpaka huu sasa wanalazimika kukimbia mashambulizi ya anga, mizinga mizito, makombora na milio ya risasi,” alisema.

Makazi ya hifadhi Beirut yamefurika – IOM

Kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), Mkuu wa ofisi hiyo nchini Lebanon, Mathieu Luciano, ameeleza kuzorota kwa hali nchini humo Alhamisi jioni wakati jeshi la Israel lilipofanya “mashambulizi mengi ya anga katika kitongoji cha kusini cha Beirut usiku kucha.”

Ameongeza kuwa makazi mengi ya pamoja yamejaa, hasa Beirut na Mlima Lebanon, “hivyo watu wanaelekezwa katika makazi mengine, hasa kaskazini, Al Qaa na maeneo salama katika Bekaa, ambako bado kuna nafasi.”

Watu wanakimbilia Asia ya Kusini na Magharibi – UNHCR

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa mgogoro unaoongezeka ni dharura kubwa ya kibinadamu inayohitaji hatua za haraka za kikanda.

Mkurugenzi wa Dharura wa UNHCR, Ayaki Ito, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa mzozo huo unasababisha watu wengi kuhamia maeneo mbalimbali katika kanda hiyo na kuelekea Asia ya Kusini Magharibi.

Takribani watu milioni 25 katika maeneo yaliyoathirika tayari ni wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi au waliorejea hivi karibuni, hali inayoongeza shinikizo kwa nchi zinazowahifadhi ambazo tayari ni dhaifu.

Madhara ya kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz

Mgogoro mkubwa wa usafirishaji wa kibiashara uliosababishwa na vita, ambao kwa kiasi kikubwa umesimamisha harakati za meli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kusini mwa Iran, tayari unaathiri mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaojaribu kusafirisha misaada ya kuokoa maisha kwenda Gaza na Sudan, miongoni mwa maeneo mengine yenye dharura.

Njia hiyo nyembamba ya bahari hubeba karibu asilimia 20 ya mafuta yote duniani pamoja na kiasi kikubwa cha bidhaa za kibiashara.

“Usafiri wa baharini umepungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Anne Schaefer, Naibu Mkurugenzi wa IOM anayehusika na mwitikio wa kibinadamu na uokoaji akiongeza kuwa “hali hii inaonekana katika Bandari ya Sudan, lakini pia katika bandari nyingine barani Afrika.”

Kwa upande wa Gaza, vifaa vya makazi kama turubai, mahema na taa “vimekwama katika hatua mbalimbali na haviwezi kufika kwa sasa,” amesema, akionya kuhusu “kuzorota kwa haraka sana kwa mnyororo wa usambazaji.”

Madhara kwa operesheni za misaada nchini Sudan pia ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa kwani hali ya kibinadamu “inazidi kuwa mbaya haraka sana,” ameendelea kueleza afisa wa IOM. “Na bila shaka msimu wa mvua unakaribia, hivyo ikiwa hatutapeleka vifaa katika wiki sita hadi nane zijazo, itakuwa vigumu sana kuwafikia watu, hasa katika Darfur.”

Vifaa vya matibabu vinasafirishwa kwa ndege kutoka Dubai- WHO

Akisisitiza wasiwasi huo, Dkt. Hanan Balkhy, Mkurugenzi wa Kanda wa WHO kwa Mashariki ya Mediterania, amethibitisha kuwa vifaa muhimu vya tiba havipitishwi kupitia Mlango wa Hormuz. Hata hivyo amebainisha kuwa safari za ndege zimeanza tena kutoka Dubai, ambayo ni kitovu kikubwa cha usafirishaji kwa mfumo mzima wa misaada ya kibinadamu.

“Tuna zaidi ya maombi 50 ya vifaa vya dharura katika nchi 25 zilizoathiriwa na kusitishwa huku kwa sasa,” amesema Dkt. Balkhy, akitaja Lebanon, Yemen na Somalia miongoni mwa nchi hizo.

Kauli ya Türk kwa nchi husika

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi amezihimiza nchi zinazohusika kuchukua hatua za haraka za kupunguza mvutano ili kuipa amani nafasi na pia akasema, “nazihimiza nchi nyingine kuzitaka waziwazi pande zinazohusika kujizuia na kurudi nyuma. Busara na utulivu lazima vitawale ikiwa tunataka kuzuia hofu na uharibifu zaidi kwa raia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *