Watu 23 wamepoteza maisha jijini Nairobi nchini Kenya, kwa mujibu wa ripoti za polisi, kufuatia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko usiku kucha kuamkia siku ya Jumamosi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Barabara nyingi za jiji la Nairobi, ziligeuka kuwa mito kwa sababu ya mafuriko, ambayo yamesababisha maafa na kuathiri makaazi ya maelfu ya watu, huku wenye magari wakisombwa na maji katika barabara kadhaa hasa ile ya kwenda Mombasa.
Hadi siku ya Jumamosi, maafisa wa uokoaji, wamekuwa wakijaribu kuwaokoa watu waliokwama kwa sababu ya mafuriko katika barabara ya Kirinyaga na mitaa ya kifahari kama Parklands, wakiopoa miili ya watu walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mbali na watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha, polisi wanasema wamewaokoa watu wengin karibu 30 usiku wa kuamkia Jumamosi, wakati huu msako zaidi ukiendelea.
Shirika la ndege nchini Kenya, limeamua kuhamishia baadhi ya ndege zilizotakiwa kutoa jijini Nairobi hadi jijini Mombasa kwa sababu ya mvua kubwa.
Mvua kubwa inapoendelea kunyesha jijini Nairobi na maeneo mengine ya nchi hiyo, mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa inaonya kuwa kiwango cha mvua kitaendelea kuongzeka na kuwataka wakaazi wa jiji hilo na maeneo mengine kuhamia maeneo yaliyoinuka.