ACI FMA yajipanga kuimarisha masoko ya fedha, yaiunga mkono Dira 2050ACI FMA yajipanga kuimarisha masoko ya fedha, yaiunga mkono Dira 2050

Dar es Salaam. Chama cha wataalamu wa masoko ya fedha nchini, ACI FMA Tanzania kimesema kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha maendeleo ya masoko ya fedha na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Rais wa chama hicho, Farid Ally ameyasema hayo wakati wa hafla ya futari iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, iliyowakutanisha wadau wa soko, watunga sera na wadhibiti wa sekta ya fedha kujadili maendeleo na changamoto zinazokabili masoko ya fedha nchini.

Amesema kupitia ushirikiano wa karibu na wadhibiti, watunga sera na wadau wa sekta hiyo, chama hicho kitaendelea kuunga mkono mipango inayolenga kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania, ikiwemo azma ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

“ACI FMA Tanzania kama chombo cha kitaaluma kinachowakilisha wataalamu wa masoko ya fedha kinatambua jukumu lake katika kuimarisha maendeleo na uadilifu wa masoko ya fedha nchini,” amesema Ally.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Peter Nalitolela (kulia) akizungumza wakati wa mjadala uliofanyika pamoja futari iliyoandaliwa na ACI FMA Tanzania jijini Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa kuimarisha ushirikiano na watunga sera pamoja na wadhibiti ni sehemu muhimu ya juhudi za kukuza kanuni bora za uendeshaji wa soko na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Katika hafla hiyo, wadau walipata fursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya masoko ya fedha nchini, ikiwemo ukosefu wa utofauti wa bidhaa za kifedha, taratibu ngumu za udhibiti kwa washiriki wapya wa soko pamoja na utegemezi mkubwa wa ufadhili kutoka taasisi za kifedha.

Akizungumzia hali ya soko la mitaji nchini, Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela amesema ingawa soko hilo linaendelea kukua, bado uelewa wa wawekezaji wadogo kuhusu fursa zilizopo ni mdogo.

Amesema licha ya idadi ya akaunti za mfumo wa Central Depository System (CDS) kuwa ndogo, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wawekezaji wapya wanaoanza kuingia katika soko la hisa.

“Ingawa kuna ongezeko la watu wanaotaka kuwekeza katika soko la hisa, changamoto bado zipo, zikiwemo ukosefu wa utofauti wa bidhaa za kifedha na maandalizi ya soko kukidhi ongezeko la ushiriki wa wawekezaji,” amesema Nalitolela.

Pia amesema kupungua kwa mauzo ya awali ya hisa kwa umma (IPO) si tatizo la Tanzania pekee bali ni mwenendo unaoonekana katika masoko mengi duniani.

Hata hivyo, amesema Tanzania inaendelea kubadilika kutoka katika mfumo wa uchumi unaoongozwa zaidi na serikali kuelekea uchumi unaochochewa na sekta binafsi, hali inayotarajiwa kuimarisha zaidi masoko ya mitaji na hisa.

Wakati huo huo, Rais wa ACI FMA Duniani, Rui Correia ametangaza mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanawake barani Afrika ili kusaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya masoko ya fedha.

Amesema mpango huo utaanza mwaka huu kwa kuwalenga wanawake barani Afrika na unatarajiwa kusaidia kukuza uwezo wa kitaaluma kwa wataalamu wanawake katika sekta hiyo.

“Elimu siyo kupata vyeti pekee, bali ni kubadilishana utaalamu, maarifa na uzoefu katika nyanja mbalimbali za masoko ya fedha,” amesema Correia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *