
Nchini Burkina Faso, shambulio jipya limelenga vikosi vya usalama siku ya Ijumaa, Machi 6. Shambulio hilo liliwalenga maafisa kutoka GUMI (Kikosi cha msaada wa haraka), kilichopo Yamba, yapata kilomita 20 kutoka Fada N’Gourma mashariki mwa nchi. Kambi yao iliporwa na kuchomwa moto. Hakuna idadi rasmi ya vifo ambayo imetolewa kwa sasa, lakini kulingana na vyanzo vya usalama, angalau maafisa 30 wa polisi waliuawa katika shambulio hilo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Washambuliaji walifika kwa wingi wakiwa na pikipiki alasiri ya Ijumaa, Machi 6. Shambulio hilo lilidumu kwa angalau saa mbili, kulingana na chanzo cha usalama. Kambi ilivamiwa na baadhi ya vifaa vilichukuliwa na magaidi, chanzo hicho kimeongeza. Chanzo kingine kimesema kwamba arifa zilitolewa mara kwa mara, lakini askari waliotumwa kusaidia hawakufika kwa wakati. Shambulio hilo lilitokea wakati timu mpya ya mafisa wa polisi ilikuwa ikichukuwa nafasi ya ile ya awali.
Hakuna takwimu rasmi za majeruhi zinazopatikana kwa wakati huu. Vyanzo vilivyowasiliana nasi vinaripoti kuwa dazeni kadhaa walifariki na kujeruhiwa miongoni mwa maafisa wa polisi. Operesheni ya kuwatafuta majeruhi na miili ya maafisa wa polisi waliouawa inaendelea na hasa kwa wale ambao bado hawajulikani waliko.
Kambi hiyo ilikumbwa na shambulio kama hilo mwaka jana, karibu wakati huo huo. Tangu mwanzoni mwa mwaka, eneo la mashariki mwa Burkina Faso, linalopakana na Benin, Togo, na Niger, limekuwa likilengwa na makundi ya kigaidi. Wiki mbili zilizopita, kikosi cha walinzi wa misitu huko Tandjari kilishambuliwa, na pia kusababisha vifo vya watu kadhaa.