Dar es Salaam. Jumuiya ya Waislamu wa Shia nchini wamejumuika na makundi mengine kuomboleza kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei huku wakimwelezea kama mtu aliyehubiri amani na kuwaunganisha watu.

Hayo yamebainishwa leo Machi 8, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla maalumu iliyowakutanisha wadau na washirika mbalimbali wa Iran katika hafla ya maombolezo ya kiongozi wao.

Khamenei aliuawa Februari 28, 2026 kutokana na mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Marekani kwa ushirikiano na Israel ambapo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, maelfu kujeruhiwa na wengine kupoteza makazi yao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani  nchini, Sheikh Alhad Mussa Salum amesema   mizozo inayoendelea Mashariki ya Kati haina afya kwa ulimwengu mzima kwani amani ikitoweka athari zake ni kubwa.

Amesema ni wakati sasa kwa pande zinazokinzana kukaa mezani kuzungumza na kufikia makubaliano ya kuweka silaha chini ili amani iendelee kudumu siku zote.

“Haya yanayoendelea leo yanahatarisha usalama wa dunia nzima na athari zitaendelea sio Mashariki ya Kati bali ulimwengu mzima.

“Ni jambo jema kwamba nchi zinazogombana zikae zizungumze ili kufikia mwafaka na jambo hili liishe,” amesema Sheikh Alhad.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Mohamed Javad Hemmatpanah ameishukuru Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokea kuomboleza pamoja nao kufuatia kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

“Viongozi mbalimbali wa Serikali na Watanzania wamefika kwenye makazi yetu kutoa rambirambi zao, tunawashukuru kwa mshikamano mkubwa waliotuonyesha,” amesema Balozi Hemmatpanah.

Kwa upande wake, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tabora, Isaya Mugaragu amesema waislamu wamempoteza kiongozi ambaye alikuwa mpigania amani duniani pamoja na mshikamano kwa watu wote.

“Kwa mujibu wa UN Charter (Mkataba wa Umoja wa Mataifa), hakuna taifa lenye mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Hiki kilichofanyika Iran siyo sawa, ni tishio la amani ya ulimwengu,” amesema.

Mchungaji Mugaragu amesisitiza kwamba Khamenei alikuwa akipenda amani ndiyo maana alipendwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mwaka 1985 alifanya ziara hapa Tanzania.

Ameutaka ulimwengu kusimama pamoja kupinga mashambukizi hayo dhidi ya Iran kwani ni tishio la amani ya dunia na ubinadamu. Amezitaka Marekani na Israel kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Naye mkufunzi wa Chuo cha Kimataifa cha Jamae al-Mustafa, Gawth Nyambwa amesema kuuawa kwa Khamenei siyo tu ni pigo kwa Wairan, bali kwa ulimwengu mzima kwa sababu alikuwa akipigania amani na ameshiriki shughuli za maendeleo.

“Khamenei hakuwahi kupigania vita na taifa lolote na alikuwa akishiriki shughuli za maendeleo kwenye mataifa mbalimbali. Vyuo kama hiki, amejenga vingi sana,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *