Fujo za aina yake zimeibuka mwishoni mwa mchezo wa fainali ya michuano ya jimbo la Minas Gerais nchini Brazil kati ya Cruzeiro dhidi ya Atletico Mineiro na kusababisha jumla ya kadi nyekundu 23 kutolewa.
Katika mchezo huo uliochezwa usiku wa kumkia leo,Jumatatu kwenye uwanja wa Mineirao, Cruzeiro ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0, lilofungwa na Kaio Jorge.
Mwamuzi wa mchezo huo, Matheus Delgado Candançan, alieleza katika ripoti rasmi ya mechi kuwa ugomvi ulianza baada ya mvutano kati ya kipa wa Atletico, Everson na kiungo wa Cruzeiro, Christian.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Everson alionekana kuchukia baada ya kuchezewa faulo na kisha kumuangusha mpinzani wake kabla ya kumpiga usoni. Baada ya tukio hilo ndipo vurugu hizo zilipoibuka.
Mwamuzi pia alieleza kuwa Christian alimkanyaga Everson kichwani wakati mpira tayari ulikuwa mikononi mwa kipa huyo, jambo lililochochea zaidi ugomvi huo.
Baada ya hapo, wachezaji wa timu hizo waliamua kuzichapa, hali iliyosababisha mwamuzi kushindwa kutoa kadi papo hapo kutokana na vurugu zilizokuwa zinaendelea.
Kwa upande wa Cruzeiro, wachezaji 12 wameonyeshwa kadi nyekundu akiwemo kipa Cassio pamoja na mfungaji wa bao Kaio Jorge. Kwa upande wa Atlético Mineiro, wachezaji 11 nao wamepewa umeme wakiongozwa na kipa Everson na mshambuliaji nyota Hulk.
Sehemu ya ugomvi uliozuka jana Machi 8, 2026 katika mechi ya fainali michuano ya Jimbo la Minas Gerais nchini Brazil kati ya Cruzeiro dhidi ya Atletico Mineiro. Picha na Mtandao
Fujo hizo zilisababisha mchezo kusimama kwa dakika 10 kabla ya polisi kuingia uwanjani na kutuliza mvutano huo. Baada ya utulivu kurejea, mwamuzi aliamua kumaliza mechi hiyo.
Ushindi huo uliifanya Cruzeiro kumaliza ukame wa miaka saba bila kutwaa ubingwa wa Campeonato Mineiro.
