Liverpool, England. Beki wa kushoto wa Liverpool, Andy Robertson, amesema aliamua kukataa ofa ya kujiunga na Tottenham Hotspur katika dirisha la usajili la Januari kwa sababu bado anataka kuendelea kuitumikia Liverpool hadi pale klabu itakapohisi haihitaji huduma yake.
Nyota huyo wa Scotland mwenye umri wa miaka 31 amethibitisha kuwa kulikuwa na mazungumzo kati ya pande zote mbili wakati Tottenham walipokuwa wakitafuta wachezaji wa kuimarisha kikosi chao katika dirisha la majira ya baridi.
“Ni kweli kulikuwa na mazungumzo kati ya klabu zote mbili, lakini mwisho wa siku niliamua kubaki Liverpool,” amesema Robertson baada ya kufunga bao katika ushindi wa Liverpool dhidi ya Wolves kwenye Kombe la FA.
Robertson amesema amekuwa mwaminifu kwa Liverpool tangu alipojiunga mwaka 2017 na ana mpango wa kuendelea hivyo.
“Nimekuwa na dhamira kwa Liverpool kwa miaka karibu tisa sasa, na nitaendelea kuwa na dhamira hiyo hadi nitakapokuwa sihitajiki tena,” amesema.
Beki wa kushoto wa Liverpool, Andy Robertson, akizungumza baada kumalizika kwa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Wolverhampton iliyopigwa Machi 6, 2026. Picha na Mtandao
Ameongeza kuwa klabu hiyo imempa kila kitu katika maisha yake ya soka, na yeye pia ametoa kila kitu kwa ajili ya mafanikio ya timu.
Hivi sasa Robertson anakabiliwa na ushindani mkali katika nafasi ya beki wa kushoto, ambapo mchezaji mpya Milos Kerkez ameonekana kupata nafasi zaidi katika kikosi.
Hata hivyo, Robertson amesema ataendelea kujituma kila anapopewa nafasi uwanjani au mazoezini.
Mkataba wa Robertson na Liverpool unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, na bado haijajulikana kama pande zote zitafikia makubaliano ya mkataba mpya.
Beki wa kushoto wa Liverpool, Andy Robertson, akishangilia baada ya kufunga bao katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Wolverhampton iliyopigwa Machi 6, 2026. Picha na Mtandao
“Uamuzi utakapofanywa, mtatangaziwa. Kwa sasa bado nina miezi mitatu tu katika mkataba wangu,” amesema Robertson.
Amesisitiza kuwa lengo lake kuu ni kushinda mataji akiwa Liverpool, ikiwemo Kombe la FA, Carabao, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England.
“Lengo langu limekuwa kushinda mataji kila msimu kwa sababu hilo ndilo ambalo klabu na mashabiki wanataka,” amesema.
Kwa sasa Robertson amesema akili yake yote ipo katika kusaidia Liverpool kumaliza msimu kwa mafanikio kadri iwezekanavyo.
