
Yakitambuliwa kama Hitimisho Lililokubaliwa au Agreed Conclusions, nyaraka hiyo imepitishwa kwa makubaliano mapana wakati wa ufunguzi wa CSW70, ambao ni mkutano mkubwa wa Umoja wa Mataifa unaojikita katika usawa wa kijinsia na haki za wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumanne na UN Women jijini New York, Marekani, nyaraka inaweka mwongozo wa hatua za kuimarisha mifumo ya sheria na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki kwa usawa duniani.
Nyaraka ni kiashiria cha dhamira za serikali
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Sima Bahous, amekaribisha hatua hiyo akisema makubaliano hayo yanaonesha dhamira za serikali za kumaliza kutokuchukuliwa hatua dhidi ya wahalifu na kujenga mifumo ya haki inayowahudumia watu wote kwa usawa.
Mwenyekiti wa CSW70, Maritza Chan wa Costa Rica, amesema jukumu kubwa sasa ni kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa, akisisitiza kuwa nyuma ya takwimu zote za ukosefu wa usawa kuna maisha halisi ya wanawake na wasichana wanaosubiri kuona kama viongozi watatekeleza wanachokiahidi.
Kinachotarajiwa kutekelezwa na serikali
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa hadi sasa hakuna nchi iliyofikia usawa kamili wa kisheria kati ya wanawake na wanaume.
- Kupitia makubaliano hayo, serikali zimehimizwa kuchunguza na kurekebisha sheria zinazobagua wanawake, ikiwemo zile zinazohusu ndoa za utotoni, sheria za familia na haki za kumiliki mali.
- Pia zinatakiwa kuchukua hatua kali zaidi kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, mtandaoni na nje ya mtandao, pamoja na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa na manusura wanapata msaada na haki kwa wakati.
- Mapendekezo mengine muhimu ni pamoja na kupanua upatikanaji wa msaada wa kisheria, kuimarisha uratibu kati ya taasisi za haki, kutumia teknolojia kwa uwajibikaji katika mifumo ya sheria, na kutambua rasmi wafanyakazi wa haki za jamii na wasaidizi wa kisheria katika mifumo ya kitaifa.
Mkutano wa CSW70 unafanyika kuanzia tarehe 9 hadi 19 Machi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ukileta pamoja wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia na wadau wengine kujadili sera, rasilimali na uwajibikaji ili kuharakisha usawa wa kijinsia duniani.
Soma nyaraka kamili hapa.