Miongoni mwa washiriki wa mkutano huu ni Elizabeth Waliuba, mwanzilishi na mkurugenzi wa shirika la Imarisha Usawa kutoka Kenya, ambaye anasisitiza umuhimu wa kubadili sera kuwa vitendo vinavyogusa maisha ya wanawake na wasichana katika jamii.
Kutoka kwenye sera hadi vitendo
Kwa Elizabeth Waliuba, mkutano wa mwaka huu unapaswa kuwa kichocheo cha mabadiliko halisi badala ya majadiliano pekee. Anasema nchi nyingi tayari zina sera nzuri, lakini changamoto kubwa imekuwa utekelezaji wake katika ngazi ya jamii.
“Tuko na sera nyingi sana na makubaliano mengi yaliyoandikwa, lakini sasa ni wakati wa kutoka kwenye majengo ya kutunga sera na kupeleka vitendo vyetu katika jamii,” anasema.
Akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili Elizabeth amesema kwa mtazamo wake, mabadiliko ya kweli yataonekana pale ambapo makubaliano yanayopitishwa katika mikutano ya kimataifa yatawafikia wanawake na wasichana katika maisha yao ya kila siku.
Jukwaa la sauti za wanawake duniani
Maudhui ya CSW70 mwaka huu ni “Haki, haki ya kisheria na hatua kwa wanawake na wasichana wote.” Kwa Waliuba, mkutano huu una umuhimu mkubwa kwa sababu unaleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali wanaoshirikiana katika ajenda ya usawa wa kijinsia.
“Kongamano hili linanionesha kwamba sifanyi kazi peke yangu, mashirika ya kiraia, serikali na watu binafsi wamekuja pamoja kuzungumzia masuala muhimu yanayogusa wanawake na wasichana,” anaeleza.
Anaamini nguvu ya mkutano huo ipo katika ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo kutoka kwa wadau wanaotoka katika mazingira na uzoefu tofauti.
Hofu ya makubaliano kubaki kwenye vitabu
Hata hivyo, Waliuba anaonya kwamba makubaliano yanayopitishwa katika mikutano ya kimataifa mara nyingi hubaki kwenye karatasi bila utekelezaji madhubuti.
Anasema “Matarajio yangu ni kwamba tutakapotoka hapa, maamuzi yatakayopitishwa hayatabaki kwenye vitabu au nyuma ya milango iliyofungwa; tunataka yaende kwenye jamii na tuone hatua halisi”.
Kwa mujibu wake, katika nchi kama Kenya changamoto si ukosefu wa sera, bali ni upungufu wa utekelezaji unaogusa maisha ya wanawake na wasichana.
Michezo kama daraja la kuwafikia wasichana
Kupitia shirika lake la Imarisha Usawa, Waliuba anatumia mbinu bunifu kufikisha ujumbe wa haki na usawa kwa wanawake na wasichana. Moja ya njia hizo ni kutumia michezo, hasa mpira wa kikapu, kama jukwaa la majadiliano na elimu.
“Tulichagua mchezo wa mpira wa vikapu kwa sababu ni mahali ambapo wasichana na wanawake wanahisi wako salama na wanaweza kuzungumza bila uoga,” anasema.
Ameongeza kuwa michezo pia ina uwezo wa kuwaunganisha watu kutoka rika na mazingira tofauti, na hivyo kujenga majadiliano ya wazi kuhusu haki, usawa na changamoto zinazowakabili wanawake.
Wito kwa wanawake kupaza sauti
Mwisho wa mahojiano, Waliuba anatoa ujumbe kwa wanawake duniani kote, akisisitiza umuhimu wa kutumia nafasi walizonazo kuleta mabadiliko.
“Wanawake tunaweza. Tunahitaji kupaza sauti zetu, na wale walio katika nafasi za maamuzi watumie sauti zao kushawishi mabadiliko yanayowahusu wanawake na wasichana,” anasema.
Kwa mujibu wake, uhuru wa wanawake kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa na kijamii ni hatua muhimu kuelekea usawa wa kweli.
Kadri mkutano wa CSW70 unavyoendelea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, washiriki kama Elizabeth Waliuba wanatumai kwamba mijadala na maamuzi yatakayofikiwa yatachochea hatua madhubuti si tu katika sera, bali katika maisha halisi ya wanawake na wasichana duniani.