
Dar es Salaam. Wataalamu zaidi ya 600 wa sekta ya ujenzi na upangaji miji wanatarajiwa kukutana mkoani Morogoro Aprili 9 hadi 10, 2026 kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya miji, matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa katika taaluma zao.
Mkutano huo wa siku mbili utawakutanisha wataalamu kutoka fani 12, wakiwemo wabunifu majengo, wakadiriaji majenzi, wahandisi, wapanga miji, wakandarasi na wasimamizi wa miradi.
Rais wa Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania (AAT), Meck T’chawi amesema mkutano huo unalenga kupeana ujuzi na uzoefu pamoja na kujadili namna ya kutumia maendeleo ya teknolojia ili kuendana na mahitaji ya sasa katika sekta ya ujenzi na maendeleo ya miji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 11, 2026 jijini Dar es Salaam, T’chawi pia amezungumzia changamoto ya mpangilio wa miji, akieleza kuwa ongezeko la watu ndilo linalofanya baadhi ya miji, hususan Dar es Salaam, kuonekana kama haikupangwa vizuri.
“Miji yote nchini imepangwa vizuri. Ukweli ni kwamba mipango ya miji ilianza tangu enzi za utawala wa Wajerumani hadi sasa, lakini ongezeko kubwa la watu ndilo linafanya ionekane kama haikupangwa vizuri,” amesema T’chawi.
Ameeleza kuwa katika shughuli za ujenzi, wabunifu majengo hutumia ramani zilizoandaliwa na Wizara ya Ardhi kupitia kitengo cha upangaji miji.
T’chawi, ambaye pia ni rais wa Wabunifu Majengo Afrika Mashariki (EAIA), amesema mkutano huo wa mwaka utahusisha wataalamu kutoka fani mbalimbali ikiwemo wabunifu wa ndani (Interior Designers), wabunifu wa mandhari (Landscape Architects), wabunifu wa teknolojia, wakadiriaji majenzi, wasimamizi wa ujenzi, wasimamizi wa miradi, wahandisi, wapanga miji, wakandarasi na waendelezaji majengo.
Wengine ni wahadhiri, wahitimu pamoja na wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu.
Amesema kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Upangaji na Uendelezaji Miji Ulioandaliwa kwa Miji Inayobadilika.”
T’chawi ameongeza kuwa kuna uwezekano wa kuboresha mpangilio wa Jiji la Dar es Salaam iwapo wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, wawekezaji na wataalamu watashirikiana.
“Uwezekano wa kulirejesha jiji lionekane katika mpangilio mzuri upo, iwapo wataalamu wa fani husika watatumika kikamilifu,” amesema.
Kwa upande wake, mkadiriaji majenzi kutoka Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS), Catherine Bhoke amesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na yamehusisha taasisi mbalimbali zinazofanya kazi katika sekta ya ujenzi.
Amesema wakadiriaji majenzi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha gharama za miradi ya ujenzi zinapangwa kwa usahihi.
“Huwezi kujenga kitu bila kujua gharama zake zitakuwaje. Hivyo wakadiriaji majenzi ni muhimu katika kuandaa bajeti sahihi za miradi ya ujenzi,” amesema Bhoke.
Makamu wa rais wa AAT, Fortunata Msakamali amesema zaidi ya wataalamu 600 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki mkutano huo.
Amesema kupitia mkutano huo, wataalamu hao watajifunza mbinu mbalimbali za kupanga na kuendeleza miji kwa njia endelevu ili kuhakikisha miji inakuwa salama na rafiki kwa maendeleo ya sasa na ya baadaye.
Naye Katibu Mtendaji wa AAT, Attie Ally alisema semina hiyo pia itatoa nafasi kwa wataalamu kujifunza namna ya kutumia teknolojia mpya katika sekta ya ujenzi.
“Teknolojia inaendelea kukua kwa kasi na hata vifaa vya ujenzi vinabadilika, hivyo ni muhimu wataalamu kuendelea kunolewa ili kuendana na mabadiliko hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Aprili 11, 2026 washiriki watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza utalii nchini.