
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesema katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kuwa, kufumbia macho au kutochukua hatua za maana mkabala wa vitendo vya kivamizi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kutafungua njia ya kushadidi ukosefu wa utulivu na taharuki katika eneo.
Sayyid Abbas Araghchi amesema Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo zinapasa kutoa msimamo wa nguvu na kulaani wazi wazi uvamizi na jinai zinazofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza bayana kuwa: Katika mashambulizi hayo ya kichokozi, maeneo ya kiraia kama shule, hospitali, majengo ya makazi ya watu, pamoja na majengo na makavazi yenye turathi za kihistoria yamelengwa.
Amesisitiza kuwa, vitendo hivyo vya tawala za Marekani na Israel vinaashiria ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na kanuni za msingi za sheria za ubinadamu.
Waziri Araghchi amekumbusha kuwa, kwa mara ya pili ndani ya miezi tisa, tawala za Marekani na Israel zimeanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran katikati ya mazungumzo hasasi ya kidiplomasia. Ameeleza bayana kuwa: Umoja wa Mataifa unabeba dhima ya kisheria na kimaadili ya vita haramu na vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislami ina haki na wajibu wa kuendelea kujihami na kulinda mamlaka yake ya kujitawala, hadi itakapohakikisha kuwa mashambulizi mengine dhidi yake hayakaririwi tena.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hakuna shaka kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kujihami na kulinda. Aidha amesisitizia haja ya kuheshimiwa misingi ya sheria za kimataifa, na kuchukuliwa hatua za kuzuia kuenea migogoro na matokeo mabaya ya kiusalama na kibinadamu ya vita hivyo katika eneo.