Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil amesema ujumuishaji wa kifedha unapaswa kwenda zaidi ya kutoa huduma za kifedha pekee na badala yake uwe chachu ya kuchochea uzalishaji na fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza jana Machi 11, 2025 katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NCBA Tanzania visiwani Zanzibar, Akil alisema taasisi za kifedha zina nafasi muhimu katika kusaidia ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kupata mitaji na huduma zinazosaidia kukuza shughuli zao za uzalishaji.
“Ujumuishaji wa kifedha haupaswi kuishia kwenye upatikanaji wa huduma pekee. Unapaswa pia kusaidia uzalishaji na fursa za kiuchumi. Taasisi za kifedha zinapowawezesha wasafirishaji, wazalishaji na wajasiriamali, zinasaidia kuimarisha mnyororo wa ugavi, kuunda ajira na kukuza uchumi,” alisema.
Alisema juhudi za taasisi za kifedha katika kuimarisha huduma zao zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo walioko maeneo ya mbali ambapo awali hawakuwa na fursa ya kupata huduma hizo.
Akil pia alitambua mchango wa huduma za kifedha za kidijitali ambazo zimeongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kusaidia wananchi kuweka akiba, kufanya miamala na kuendesha biashara zao kwa urahisi zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Tanzania, Alex Mziray, Mkuu wa Idara ya Masoko ya Kimataifa wa benki hiyo, Rahim Suleiman, alisema taasisi hiyo inaendelea kuweka mikakati inayolenga kusaidia ukuaji wa biashara na ustawi wa jamii kupitia huduma bunifu za kifedha.
Alisema licha ya kuwa mwezi wa Ramadhan ni kipindi cha kiroho na tafakari, shughuli za biashara na uzalishaji zinaendelea, hivyo taasisi za kifedha zina jukumu la kuhakikisha mifumo yao inaendelea kusaidia mahitaji ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
“Katika NCBA tunaamini benki inapaswa kuwa zaidi ya taasisi ya kutoa huduma za kifedha. Tunataka kuwa mshirika wa maendeleo kwa wateja wetu kwa kuwasaidia kupata mitaji, vifaa vya uzalishaji na suluhisho nyingine za kifedha zinazochochea ukuaji wa biashara,” alisema.
Aliongeza kuwa kupitia huduma za ‘Asset Finance’, benki hiyo imekuwa ikisaidia wafanyabiashara kupata magari, mitambo na vifaa vinavyowezesha uzalishaji katika sekta mbalimbali kama usafirishaji, ujenzi na biashara.
Aidha, benki hiyo inaendelea kupanua huduma zake za ‘Bancassurance’, zinazolenga kusaidia kulinda familia na biashara dhidi ya hatari zisizotarajiwa, hivyo kuimarisha ustahimilivu wa kifedha kwa muda mrefu.
Hafla hiyo ya futari iliwaunganisha wadau mbalimbali wa biashara, wajasiriamali na washirika wa maendeleo katika mazingira ya mshikamano, huku ikitoa fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu namna taasisi za kifedha zinavyoweza kuendelea kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.