
Seneta wa Marekani amekosoa uongo wa kukaririwa wa serikali na jeshi la nchi hiyo na kusema serikali imetudanganya kuhusu shambulizi lililolenga shule ya watoto wadogo nchini Iran.
Tarehe 28 Februari serikali ya Marekani ilikiuka sheria zote za kimataifa na kushambulia shule ya Minab katika mkoa wa Hormuzgan (kusini mwa Iran) ambapo wanafunzi karibu 170 wa kike na walimu 20 wa shule hiyo ya msingi waliuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Seneta Bernie Sanders ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: Jumamosi iliyopita Donald Trump alituambia kwamba shambulizi dhidi ya shule ya msingi nchini Iran lililoua watu wasiopungua 175, wengi wao wakiwa watoto wadogo, lilifanywa na Iran. Bernie Sanders ameendelea kusema: “Sasa jeshi limekiri kwamba shambulio hilo lilifanywa na Marekani. Kama wanaweza kusema uongo kuhusu suala la wazi kabisa kama hili, ni kuhusu masuala yepi mengine ambako hawajasema uongo?
Itakumbukwa kwamba Rais Donald Trump wa Marekani Jumatano iliyopita alikwepa kubeba dhima ya kuhusika na shambulizi lililolenga watoto wa kike wa shule ya msingi ya Minab nchini Iran akidai kuwa hana habari yoyote kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kijeshi unaoonyesha kwamba jeshi la Marekani ndilo lililohusika na shambulizi la mauaji katika shule hiyo ya msingi.