Marekani. Waigizaji maarufu wa Hollywood, Will Smith na Chris Rock huenda wakakutana hadharani (live) kwa mara ya kwanza tangu walipokosana katika Tuzo za Oscar.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa waigizaji hao wanaeleza, kuna mazungumzo yanaendelea kati ya wawili hao kuangalia kama kuna uwezekano wa kukutana na kufanya mahojiano maalumu ambayo huenda yakarushwa katika kituo cha televisheni cha ABC News.

 Hatua ambayo inaweza kuwa fursa ya kwanza kwao kuzungumza ana kwa ana kuhusu tukio lililotikisa tasnia ya burudani duniani.

Endapo mazungumzo hayo yatafanikiwa, hii itakuwa mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana tangu walivyokosana katika usiku wa tuzo za 94th Academy Awards mwaka 2022. Hata hivyo, hadi sasa wawili hao hawajaweka wazi kuhusu kukutana kwako huku mashabiki wakidai kuwa huenda ni mbinu ya kutaka watu wasijue kwa sasa.

Ikumbukwe tukio ambalo limewafanya wawili hao wasikutane kwa takribani miaka mitatu ni baada ya Rock kufanya mzaha kwa mke wa Smith, Jada Pinkett Smith. Jambo lililopelekea Smith kushindwa kujizuia na kupanda jukwaani na kumpiga kofi mchekeshaji huyo mbele ya hadhira na watazamaji wa televisheni duniani kote.

Baada ya tukio hilo, Smith alirudi kwenye kiti chake na baadaye usiku huo akapokea tuzo ya Mwigizaji Bora kutokana na uigizaji wake katika filamu King Richard. Lakini tukio hilo liliendelea kuwa gumzo katika ulimwengu wa burudani.

Aidha baadaye Smith alimuomba radhi Rock na kwa Academy of Motion Picture Arts and Sciences. Akisema kitendo chake kilikuwa sio kizuri na hakikubaliki hata kidogo, kufuatia tukio hilo, Academy ilichukua uamuzi wa kumpiga marufuku Smith kuhudhuria hafla za tuzo za Oscar kwa miaka 10.

Katika maelezo yake baada ya tukio la kibao kwenye 94th Academy Awards mwaka 2022, Will Smith alieleza kuwa moja ya sababu iliyomfanya achukue hatua hiyo ilikuwa ni mzaha uliomhusu mke wake, Jada Pinkett Smith, ambaye anakabiliwa na ugonjwa unaosababisha kupoteza nywele unaoitwa Alopecia Areata.

Jada aliwahi kufunguka kuhusu ugonjwa huo mwaka 2018, akisema ulipelekea nywele zake kuanza kukatika zenyewe na kudondoka kidogo kidogo. Hali iliyomlazimu kunyoa kabisa nywele zake wakati wa hafla ya Oscars, mchekeshaji Chris Rock alifanya mzaha uliolinganisha muonekano wa Jada na mhusika wa filamu G.I. Jane, jambo lililomfanya Smith kuona kama lilikuwa kejeli kwa hali ya kiafya ya mke wake.

Kwa upande wa Chris Rock aligusia tukio hilo katika maonyesho yake ya stand-up comedy, hasa kwenye kipindi chake maalumu cha mwaka 2023 kilichooneshwa Netflix kiitwacho Chris Rock: Selective Outrage. Katika onyesho hilo, Rock alitoa mtazamo wake kuhusu kilichotokea, akisema tukio hilo lilimshangaza lakini alijaribu kulikabili kwa njia ya vichekesho kama ilivyo kazi yake.

Iwapo mahojiano hayo yatafanyika, yatakuwa fursa ya kipekee kwa wawili hao kujadili hadharani tukio ambalo limeendelea kukumbukwa kama moja ya matukio yaliyoacha alama kubwa katika historia ya burudani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *