Mamilioni ya wananchi wa Iran katika pembe zote za nchi wameshiriki katika maandamano makubwa ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds Ijumaa, huku tawala za kitwaghuti za Marekani na Israel zikiendelea kushambulia kwa mabomu miji mbali mbali ya Jamhuri ya Kiislamu.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee, kwani yanajiri huku vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza vikiingia katika mwezi wa 28. Tangu utawala huo katili uanzishe mauaji hayo ya halaiki ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba mwaka 2023, Wapalestina zaidi ya 72,000, aghalabu wakiwa wanawake na watoto wadogo wameuawa shahidi.

Aidha Siku ya Quds ya mwaka huu inaadhimishwa huku majeshi ya utawala wa Kizayuni na Marekani yakiendelea kushambulia kwa makombora maeneo mbali mbali ya Iran, jinai ambazo zimeilazimishwa Iran kujibu mapigo. 

Vita hivi  vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 Ramadhani kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea huku adhabu dhidi ya wavamizi ikiendelea kubaki katika ajenda kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran.

Katika mji mkuu wa Iran, Tehran, wananchi wametembea hadi katika Chuo Kikuu cha Tehran, licha ya baridi kali na pamoja na kitendo cha tawala za kigaidi za Marekani na Israel cha kuendelea kudondosha mabomu katika sehemu tofauti ya jiji.

Maandamano kama haya ya Siku ya Kimataifa ya Quds yamefanyika katika miji na mikoa mingine ya Iran, ikiwemo Isfahan, Mashhad, Shiraz, na Tabriz, ambapo waandamanaji walikuwa wamebeba picha ya Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei na bendera za Palestina na Iran.

Wananchi wa Iran kwenye maandamano hayo wamesikika wakipiga nara za ‘Mauti kwa Marekani’, na ‘Mauti kwa Israel’ huku wakitoa mwito wa kukombolewa Quds Tukufu, sambamba na kulaani kimya cha Wamagharibi mkabala wa jinai za kivita za Wazayuni.

Hali kadhalika, maandamano ya siku hii ya kulibakisha hai kadhia ya Palestina na ukombozi wa Quds Tukufu yamefanyika kieneo na kimataifa, ambapo yameshuhudiwa katika nchi tofauti za eneo hili kama Iraq, Lebanon, Yemen, Pakistan, na Bahrain, na vile vile katika miji mbali mbali ya nchi za Ulaya, Amerika na Afrika.

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoangusha utawala kiimla wa Shah aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani, Imam Rohoulah Khomeini alitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *