
Shirika la habari la Reuters limemnukuu mmoja wa washauri wa Rais wa Marekani akisema kuwa hitilafu kubwa zimepamba moto ndani ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, kuhusu mwelekeo wa vita vya sasa na Iran.
Duru za ndani ya serikali ya Marekani inayoongozwa na Donald Trump zinasema hitilafu kali zimejitokeza ndani ya utawala huo kuhusu vita vya kulazimisha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Likimnukuu mmoja wa washauri wa Trump, shirika la habari la Reuters limeandika: Hitilafu za ndani ya White House zinaathiri matamshi yanayotolewa na Rais wa Marekani kuhusu mwelekeo wa vita.”
Chanzo hicho ambacho hakikutajwa kwa jina kimeiambia Reuters kwamba, kutokana na kushadidi mapigano, washauri wa Rais wa Marekani wanajadili suala la wakati na njia ya kutumia kwa ajili ya kutangaza “ushindi katika vita n Iran”.
Ripoti hiyo inasema, baadhi ya maafisa wa White House wamemtahadharisha Donald Trump kwamba kupanda juu bei ya mafuta ya petroli kunaweza kuwa na gharama kubwa za kisiasa kwa Washington.
Afisa mmoja ameiambia Reuters kwamba baadhi ya maafisa wa serikali wenye misimamo mikali wanashinikiza kwa ajili ya kuendelezwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Vita vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari sawa na 10 Ramadhani kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea huku Jamhuri ya Kiislamu ikiendelea kutoa vipigo dhidi ya wavamizi na kushambulia ngome na maslahi ya tawala hizo mbili za kishetani katika eneo lote la Magharibi mwa Asia.