Wizara, PURA waweka mikakati utafitaji mafuta, gesi asiliaWizara, PURA waweka mikakati utafitaji mafuta, gesi asilia

Dar es Salaam: Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi asilia, Dk James Mataragio amekutana na menejiment ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam mnamo Machi 12, 2026 kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Antelimi Raphael, Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni na baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Nishati na PURA.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Dkt Mataragio alieleza kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kufanyiwa kazi kubwa katika sekta ya mafuta na gesi ni eneo la utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa kuzingatia kuwa shughuli hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Miaka ya nyuma, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zilikuwa zikifanyika kwa wingi na kasi kubwa. Tukiangalia hata mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato yani ‘PSA’, zilikuwa zaidi ya 26 lakini leo hii tunaongelea mikataba 11 pekee.

“Na ukijaribu kuangalia kwa kina, hata katika PSA zilizobaki ni kampuni chache zinatekeleza majukumu yao ya kuendelea kufanya utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Hali hili hairidhishi. Lazima tuweke mikakati inayolenga kuchochea shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini,” Katibu Mkuu alisisitiza.

SOMA: PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba gesi asilia

Kwa mujibu wa Dk Mataragio, mdororo wa shughuli za utafutaji ni hatari kwa uhakika wa upatikanaji wa gesi asilia kwa kuwa utafutaji ndio chachu ya ugunduzi ambao ukiendelezwa unapelekea uzalishaji wa gesi asilia.

“Kwa sasa tumejipanga kama Wizara kuhakikisha tunaweka jitihada kubwa katika eneo hili na kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia” aliongeza.

Kwa upande wake, Mhandisi Charles Sangweni alieleza kuwa PURA imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuingia mikataba na makampuni ya kijiofizikia yaliyobobea katika ukusanyaji wa data za petroli (Multi Client Geophysical Companies) kwa lengo la kuendeleza utafiti katika maeneo ya bahari kuu na nchi kavu.

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na PURA zilijadili kwa kina mikakati ya kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia na kuainisha masuala muhimu yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka ili kuleta uhai katika sekta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *