
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba: “Taifa la Iran, kwa umoja na mshikamano, litaendelea kusimama pamoja na misingi na malengo yake, na halitarudi nyuma kamwe.”
Sayyid Abbas Araghchi amesema pembeni mwa maandamano ya Kimataifa ya Siku ya Quds kwamba: “Wananchi wa Iran, kwa kujitokeza kwao kwa mamilioni mitaani, mjini Tehran na katika miji mingine, wameonyesha kwa wazi azma yao thabiti ya kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu, Quds, Palestina na misingi ya taifa.”
Araghchi aliongeza: “Ushiriki huu mkubwa unaonyesha dhamira na uamuzi madhubuti wa Wairani katika kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu na kadhia ya Quds. Tutaendelea kwa nguvu hizi hizi, na maadui watalazimika kutambua uwezo na nguvu ya watu wa Iran.”
Akijibu swali kuhusu kupanda kwa bei, pia amesema: “Bei ya mafuta tayari inaongezeka, na hili ni matokeo ya hatua za Marekani na Israel katika eneo hili. Wao ndio walioleta hali hii ngumu kwa eneo, na wanapaswa kuwajibishwa.”
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Iran amehitimisha kwa kusisitiza kwamba taifa la Iran, kwa umoja na mshikamano, litaendelea kuunga mkono misingi yake na halitarudi nyuma kamwe.
Mamilioni ya wananchi wa Iran katika pembe zote za nchi wameshiriki katika maandamano makubwa ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds katika Ijumaa ya mwishi ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani, huku tawala za kitwaghuti za Marekani na Israel zikiendelea kushambulia kwa mabomu miji mbali mbali ya Jamhuri ya Kiislamu.
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya mwaka huu yamekuwa na umuhimu wa kipekee, kwani yamejiri huku vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza vikiingia katika mwezi wa 28. Tangu utawala huo katili uanzishe mauaji hayo ya halaiki ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba mwaka 2023, Wapalestina zaidi ya 72,000, aghalabu wakiwa wanawake na watoto wadogo wameuawa shahidi.
Aidha Siku ya Quds ya mwaka huu imedhimishwa huku majeshi ya utawala wa Kizayuni na Marekani yakiendelea kushambulia kwa makombora maeneo mbali mbali ya Iran, jinai ambazo zimeilazimishwa Iran kujibu mapigo.
Vita hivi vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 Ramadhani kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea huku adhabu dhidi ya wavamizi ikiendelea kubaki katika ajenda kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran.