Kwa mujibu wa taarifa ya WHO iliyotolewa leo Jumapili mjini Geneva Uswisi fedha hizo zinazotokana na michango ya wafadhili zitalenga kuimarisha uratibu wa dharura, huduma za matibabu ya majeruhi na ufuatiliaji wa magonjwa, huku zikihakikisha pia upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu.

Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “Mazingira yanavyozidi kuwa mabaya na majeruhi kuongezeka, mashambulizi dhidi ya huduma za afya pia yanaongezeka na kuweka mzigo mkubwa kwenye mifumo ya afya wakati ambapo huduma hizo zinahitajika zaidi. Ninatoa wito kwa pande zote kuchagua njia ya ujasiri na kuokoa maisha, njia ya amani.”

Shinikizo kubwa kwa huduma za afya Lebanon

Nchini Lebanon, WHO inasema idadi ya majeruhi inaendelea kuongezeka kufuatia mashambulizi mapya ya Hezbollah kwa msaada wa Iran na mashambulizi makali ya kulipiza kisasi kutoka Israel yaliyolenga maeneo mengi ya kusini mwa nchi hiyo na mji mkuu Beirut. Hali hiyo imeweka shinikizo kubwa kwa huduma za afya.

Mwishoni mwa wiki, Dkt.Tedros alisisitiza kuwa kuuawa kwa wafanyakazi 14 wahudumu wa afya kusini mwa Lebanon ndani ya saa 24 ni “tukio la kusikitisha” katika mgogoro wa kikanda uliosababishwa na mashambulizi ya anga dhidi ya Iran. Madaktari 12 waliuawa katika shambulio la usiku kwenye kituo cha afya cha Bourj Qalaouiyeh, huku wahudumu wawili wa huduma za dharura wakipoteza maisha mapema katika shambulio jingine dhidi ya kituo cha afya.

Tangu Machi 2, mashambulizi 27 dhidi ya huduma za afya yamethibitishwa nchini Lebanon na kusababisha vifo vya watu 30.

Msaada pia kwa Iraq na Syria

Nchini Iraq, huduma za afya pia zinakabiliwa na shinikizo kubwa, hasa katika maeneo yaliyo karibu na maeneo ya mashambulizi na maandamano yenye vurugu. Marekani imetoa dola 500,000 kusaidia uratibu wa dharura, usimamizi wa majeruhi wengi na huduma nyingine muhimu, kwa mujibu wa WHO.

Wakati huo huo, dola 500,000 zimetengwa kwa ajili ya Syria ili kusaidia ununuzi wa dawa muhimu za kuokoa maisha na vifaa vya matibabu kwa watu waliokimbia makazi yao, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa.

Kabla ya kuanza kwa mashambulizi dhidi ya Iran, WHO ilikuwa imeomba dola milioni 633 kwa mwaka 2026 ili kukidhi mahitaji ya kanda, lakini kufikia Machi ilikuwa imepata asilimia 37 tu ya fedha hizo.

media:entermedia_image:08e83c94-ae26-49b2-a26f-be621d4cbb5f

© UNICEF Lebanon

Walinda amani wako chini ya mashambulizi

Wakati huo huo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon (UNIFIL) kusini mwa Lebanon walikumbwa tena na mashambulizi katika matukio matatu tofauti wakati wa doria mwishoni mwa wiki.

Ujumbe huo umesema risasi hizo huenda zilitoka kwa makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali karibu na vituo vyao katika  miji ya Yatar, Dayr Kifa na Qallawiyah.

“Risasi katika eneo la Yatar ziliangukia karibu sana umbali wa mita tano tu kutoka kwa walinda amani,” imesema taarifa ya UNIFIL, ikibainisha kuwa vikosi viwili vilijibu kwa kujilinda kabla ya kuendelea na shughuli zao za doria. Hakuna askari wa kulinda amani aliyejeruhiwa.

UNIFIL imesisitiza kuwa matumizi ya silaha na makundi yenye silaha ndani ya eneo lake la operesheni ni ukiukaji wa Azimio la Baraza la Usalama namba 1701, azimio lililomaliza mapigano kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006.

Wito wa kulinda raia

Ziara ya hivi karibuni ya mshikamano ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, nchini Lebanon imesisitiza pia kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa “hayakubaliki kabisa na lazima yakome.”

Akiwa mjini Beirut, Guterres alikutana na baadhi ya zaidi ya raia 800,000 waliolazimika kukimbia makazi yao tangu mapigano yaanze, akisisitiza tena kuwa raia hawapaswi kamwe kuwa shabaha ya mashambulizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *