Mkuu wa moja ya kampuni kubwa zaidi za mbolea duniani amenukuliwa na gazeti la The Guardian akionya kuwa, usambazaji wa chakula duniani utaathiriwa vibaya sana mwaka huu iwapo vita dhidi ya Iran vitapanuka na kuendelea.

Svein Tore Holsether, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Yara International ya Norway amesisitiza kuwa, kuna haja kwa viongozi wa dunia kutafakari juu ya athari za ongezeko la bei za chakula kwa nchi maskini duniani kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Amebainisha kuwa, “Kwa kuzingatia umuhimu wa pembejeo, hiki ni kitu ambacho kinaweza kuathiri vibaya uzalishaji wa mimea iwapo vita hivi vitaendelea kwa muda mrefu. Huu ni mgogoro wa kieneo wenye taathira hasi kwa dunia nzima, na unaathiri moja kwa moja mfumo wa chakula.”

Amesisitiza kuwa, iwapo Lango Bahari la Hormuz litafungwa kwa mwaka moja, hilo litakuwa janga kubwa, kwani kusimamishwa usambazaji wa pembejeo zinazohitajika kwa kilimo kutaisababishia dunia mgogoro mkubwa wa chakula.

Haya yanajiri siku chache baada ya gazeti la masuala ya kiuchumi la The Economist kuripoti kuwa, bei ya pipa moja la mafuta ya petroli itafikia dola 200 iwapo vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vitaendelea. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema, hali ya sasa inashabihiana na ile ya mwaka 2007 kabla ya kuporomoka masoko ya kimataifa.

Rais Donald Trump mpaka sasa ameshindwa kutekeleza vitisho vyake kwamba jeshi la Marekani litaishambulia Iran mara 20 zaidi ya mashambulizi ya sasa, iwapo Jamhuri ya Kiislamu itazuia meli zikiwemo za mafuta kupita katika Lango-Bahari la Hormuz.

Nchi nyingi duniani zikiwemo nchi waitifaki wa Marekani, zimesisitiza kwamba manowari za nchi zao hazitashiriki katika operesheni yoyote ya mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa katika Lango Bahari la Hormuz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *