Marufuku hospitali za serikali kuelekeza ununuzi dawa mitaaniMarufuku hospitali za serikali kuelekeza ununuzi dawa mitaani

WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ameonya vituo vya afya na hospitali za serikali kuacha tabia ya kuwaelekeza wananchi kununua dawa katika maduka ya dawa mitaani. Onyo hilo amelitoa wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nsimbo District katika viwanja vya Shule ya Msingi Songambele mkoani Katavi Region.

Dk Nchemba amesema takwimu zinaonesha kuwa kuna utoshelevu wa dawa katika vituo vya afya vya serikali, hivyo si sahihi wagonjwa kuambiwa wakazinunue nje ya hospitali. Ameeleza kushangazwa na hali hiyo na kuhoji jinsi maduka ya dawa ya mitaani yanavyoweza kuwa na dawa ambazo hospitali za serikali zinashindwa kuzipata.

Kutokana na hali hiyo, amemwelekeza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha za ununuzi wa dawa na kufahamu dawa zilizonunuliwa zimekwenda wapi. Amesisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo hivyo na hatua kali zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa dawa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaotafuta matibabu. Amesema wananchi wengi huenda hospitalini wakiwa na fedha kidogo kwa ajili ya kujiandikisha, kupata vipimo na dawa, hivyo si haki kuwaelekeza kununua dawa nje ya hospitali.

Katika hatua nyingine, Dk Nchemba amewataka viongozi kutatua migogoro ya ardhi mapema na kuepuka kuiacha iendelee kwa muda mrefu, akieleza kuwa migogoro hiyo inaweza kuhatarisha uhusiano mzuri kati ya wananchi. Ametaja migogoro kati ya wakulima na wafugaji kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka, akisisitiza kuwa ardhi haiongezeki hivyo ni lazima ipangwe na kutumika kwa utaratibu.

Pia ameonya vitendo vya utapeli wa ardhi na kusema baadhi ya wahusika wanatoka hata katika ofisi za umma, wakiwemo baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wanaotengeneza nyaraka za mikutano zenye taarifa zisizo sahihi. Amemwelekeza Mkuu wa Mkoa kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu wanaonyang’anya wananchi ardhi na kuhakikisha wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Dk Nchemba pia ameiagiza Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii kushughulikia hoja za wananchi zinazohusu matumizi ya ardhi. SOMA: Upatikanaji dawa vituo vya afya wafikia 87%

Vilevile amesisitiza haki ya malipo kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika miradi mbalimbali, akibainisha kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi kulipwa fedha za miradi lakini kushindwa kuwalipa wafanyakazi waliotekeleza kazi hizo. Amesema watu wanaobainika kufanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria hadi warejeshe fedha walizostahili kuwalipa wafanyakazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *