MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wananchi kuwa waadilifu na kulipa kodi kwa hiari, ikieleza kuwa ulipaji kodi unaweza pia kuzingatiwa kama sehemu ya ibada. Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alitoa wito huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa futari iliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
Amesema TRA inaendelea kuhamasisha utii wa sheria kwa walipakodi ili kudumisha uwajibikaji na uadilifu katika ulipaji kodi kwa hiari kama wajibu wa kiraia na kimaadili. Kwa upande wake, Abubakar Zubeir, Shehe Mkuu wa Tanzania, amewapongeza wafanyakazi wa TRA kwa juhudi zao za kukusanya kodi kwa uadilifu na kuwataka waendelee kudumisha maadili katika utendaji wao.
Amesema uaminifu na uadilifu ni nguzo muhimu katika ukusanyaji wa kodi na kwamba kufanya kazi kwa uadilifu ni sehemu ya ibada. Pia aliwataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kudumisha amani na utulivu. SOMA: Pongezi TRA, tuendelee kulipa kodi kwa maendeleo
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amewahimiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kusaidia serikali kutoa huduma kwa wananchi na kudumisha amani nchini. Ameeleza kuwa ukusanyaji wa mapato ni muhimu katika utoaji wa huduma za umma, akisisitiza kuwa bila kodi serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Msando pia amewataka wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa au huduma na kuwahimiza wafanyabiashara kutoa risiti kwa kila mauzo ili kuhakikisha uwazi katika ukusanyaji wa kodi. Aidha, amesema kumekuwa na maboresho makubwa katika utendaji wa TRA, jambo lililosababisha kupungua kwa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa awali na walipakodi.
Amebainisha kuwa ingawa changamoto bado zipo, mamlaka hiyo imekuwa rafiki zaidi kwa walipakodi na inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulipa kodi. Msando ameongeza kuwa wafanyabiashara wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi wanapaswa kuwasiliana na TRA ili kupata mwafaka wa namna bora ya kulipa kodi zao.
