MTWARA; WATAALAMU wa kilimo cha korosho nchini wameshauri wakulima kuanza kuandaa mashamba yao kwa kufuata hatua kuu tatu ili kuleta tija kwenye uzalishaji wa zao hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara, Mtafiti na Mtaalamu wa Sayansi ya Udogo na Mimea kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) kituo cha Naliendele, Abdallah Makale amesema hatua hizo kuwa ni muhimu katika kuongeza uzalishaji.
“Hatua ya kwanza ni hatua ambayo mikorosho inakuwa imetulia hasa baada ya msimu wa mavuno, ambapo ni kipindi hiki, hatua ya pili hatua ya mikorosho kuchipua na hatua ya tatu ni hatua ya uzalishaji,” amesema Makale.
Mtaalamu huyo anasema hatua ya kwanza wakulima wanapaswa kuanza kutibua mashamba yao, ili kuruhusu mikorosho ipate maji kwa ajili ya kurutubisha majani ya uzalishaji.
“Lakin pia katika hatua hii ya kwanza tunashauri wakulima kulima mazao kwenye hayo mashamba ya mikorosho na tunahimiza zaidi mazao ya jamii ya kunde kama vile karanga, choroko na kunde,” amesema.
Makale amesema kuchanganya mashamba jamii ya kunde kwenye mashamba ya mikorosho inasaidia mikorosho kupata maji na virutubisho ambavyo vinafanya maua kuwa imara kipindi kuchipua.
Hatua ya pili ni hatua ya kuchipua ambapo wakulima wanapaswa kupogolea mikorosho ili kuipa nguvu kwa kuondoa matawi ambayo yanakuwa hayazai.

Hatua ya tatu ni ya uzalishaji ambapo wakulima wanapaswa kufuatilia na kuzingatia utabiri katika kuhudumia mikorosho ikiwemo kupulizia viutilifu kudhibiti magonjwa ambayo yanaweza kuibuka wakati wa maua kuchipua na kuzaa.
Katika hatua nyingine, TARI Naliendele imeshauri wakulima kutumia mbegu bora za korosho zinazozalishwa katika kituo hicho.
Mtafiti wa mbegu Bora katika kituo hicho Dwasi Gambo amesema TARI Wana mbegu bora na miche kwa ajili ya zao la korosho.
Amesema mbegu hizo zina uwezo wa kuzalisha sana na kuhimili magonjwa na wadudu. Pia zina uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi.