
Arusha. Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zimetakiwa kujiendesha kwa misingi ya ufanisi wa kibiashara, uwazi na kujiwekea mikakati thabiti ili ziweze kutoa mchango mkubwa katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Dira ya 2050 inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka Dola za Marekani bilioni 85 hadi kufikia dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, jambo linalohitaji mchango mkubwa wa uwekezaji wa umma na binafsi, ikiwemo kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
Hayo yamesemwa jana Jumatatu Machi 16,2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Dk Khamis Mussa Omar,akifungua mkutano wa Wakurugenzi wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache (MIF 2026) unaofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Amesema ili kufikia mageuzi katika uendeshaji wa kampuni hizo ni muhimu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya uchumi wa dunia ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuimarisha uwazi.
“Dira ya 2050 inahitaji sekta ya umma na binafsi kufikiria,kufanya kazi na kusonga mbele kwa kushirikiana ili kuleta matokeo chanya kiuchumi.
Amesema bodi za wakurugenzi na menejimenti zinapaswa kuoanisha mikakati ya kampuni zao na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, huku zikizingatia mwelekeo wa masoko ya kimataifa ili kuongeza ushindani na tija ikiwemo kutumia teknolojia kuimarisha uwazi, kuongeza imani ya umma na kuboresha mifumo ya utawala bora.
Waziri huyo amesema kuna umuhimu wa kuwa na uongozi unaotazama mbele, unaoweza kutambua mapema hatari na kutumia fursa mpya katika mazingira ya ushindani wa kiuchumi na kuwa ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa mpya za uwekezaji na kuongeza matokeo chanya kwa pamoja.
Amesema wakurugenzi na watendaji wa kampuni hizo wanapaswa kutambua mapema hatari zinazoweza kujitokeza na kutumia fursa mpya katika mazingira ya uchumi wa dunia yanayozidi kuwa na ushindani mkubwa,kuimarisha mifumo madhubuti ya utawala inayozingatia uwajibikaji, uwazi na uongozi wenye maadili ni jambo la msingi katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta tija endelevu.
Amesema kuwa kampuni huzo zinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia matokeo, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kukuza faida na hatimaye kuongeza thamani kwa wanahisa pamoja na Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchambuzi wa taarifa za kiuchumi na ushindani ili maamuzi ya kibiashara yafanywe kwa kuzingatia takwimu sahihi na taarifa za soko, hatua itakayosaidia kuongeza tija na ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, akibainisha kuwa ubia imara kati ya pande hizo ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya taifa.
“Serikali kupitia Dira 2050 imejipanga kuongeza mchango wa mapato yasiyotokana na kodi katika bajeti ya taifa kutoka asilimia tatu ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ndani ya miaka mitano ijayo, sawa na lengo la kukusanya Sh 5trilioni kila mwaka,”amesema
Waziri huyo amesema kuwa mabadiliko hayo yanapaswa kwenda sambamba na matumizi bora ya kila uwekezaji katika kampuni husika ili kuweza kuleta matokeo makubwa zaidi ya kiuchumi na kifedha.
“Hii inahitaji kuondoka katika mtazamo wa usimamizi wa kawaida na badala yake kujenga uongozi unaotazama mbele, unaozingatia ubunifu, wepesi wa kufanya maamuzi na uwezo wa kutabiri mwelekeo wa maendeleo,” amesema
Awali Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Dk Fred Msemwa, ameeleza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuimarisha sekta binafsi.
Amesema wataendelea kufanya kila linalowezekana ikiwemo kupitia upya sheria na sera mbalimbali lengo likiwa ni kuboresha zaidi mazingira ya biashara, kwani wanatambua kuwa sekta binafsi ni chachu ya kufanikisha malengo ya Dira 2050.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema jukwaa hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, limekuwa sehemu muhimu ya viongozi wa kampuni hizo kujadili masuala ya utawala bora, utendaji na mchango wao katika mageuzi ya uchumi wa taifa.
Amesema kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu inayosema “Kutoka Ufuatiliaji wa kawaida hadi Uongozi wa Kimkakati unaotazama mbele:” inaakisi umuhimu wa bodi za wakurugenzi na viongozi wakuu kuacha mtazamo wa usimamizi wa kawaida na badala yake kuwa na uongozi unaoweza kutambua mapema changamoto na fursa za baadaye.
“Katika dunia ya leo inayobadilika kwa kasi kiuchumi na kiteknolojia, uongozi hauwezi tena kujikita tu katika kusimamia hali ya sasa, bali pia unapaswa kutazama mbele na kujiandaa kwa siku za usoni,” amesema.
Amesema mkutano huo pia unaendana na malengo ya Dira 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na unaochochewa na ubunifu, unaoungwa mkono na taasisi zenye ufanisi, uwajibikaji na uongozi unaotazama mbele.
Amesema kuwa uwekezaji wa Serikali katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kutoka Sh 821bilioni hadi kufikia Sh 3.6 trilioni, jambo linaloonesha kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Aidha, michango ya gawio kutoka katika kampuni hizo imeongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka Sh 58bilioni hadi kufikia Sh 266bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 357 katika kipindi hicho.
Mkutamo huo umewakutanisha zaidi ya wadau 200 wakiwemo wakurugenzi, Maofisa Watendaji Wakuu, watunga sera na wataalamu kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha utendaji na utawala wa kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, ili ziweze kuchangia kwa ufanisi zaidi katika maendeleo ya uchumi wa taifa kwa muda mrefu.