Watoto 1,688 kurejeshwa shuleniWatoto 1,688 kurejeshwa shuleni

Songwe.Halmashauri za Wilaya za Ileje na Mbozi mkoani Songwe, zimezindua mpango maalumu wa kuwarejesha shuleni watoto 1,688 wenye umri wa miaka saba hadi 17 walioko nje ya mfumo wa elimu, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).

Mpango huo unawahusisha walimu wakuu, watendaji wa kata na wenyeviti wa vitongoji, ambao wamepewa mbinu za kisasa za kuwatambua na kuwasaidia watoto waliokosa masomo kutokana na mazingira magumu na changamoto za kijamii.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, zaidi ya watoto 500 wamenufaika na uzinduzi wa mkakati huo unaoratibiwa na Idara ya Elimu ya Watu Wazima.

Ofisa Elimu ya Watu Wazima wilayani humo, Mwalimu Adelina Mwashambwa, alisema tangu mwaka 2023 hadi sasa zaidi ya watoto 3,000 wamefanikiwa kurejea shuleni kupitia mpango huo, ambao pia unatoa vifaa vya masomo bila malipo.

Amesema mafanikio hayo yameanza kuonekana, huku baadhi ya watoto waliopatiwa msaada wa kimasomo wakifanya vizuri katika mitihani yao na hivyo kuwavutia wengine kurejea shuleni.

“Mkakati huu unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Unicef, ukilenga kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu bila vikwazo,” amesema Mwashambwa.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu wilayani Mbozi, Dickson Simkwembe amewahimiza wadau kuongeza ubunifu katika kuwabaini watoto walioko nje ya mfumo wa elimu ili kuwawezesha kurejea shuleni.

Amesema viongozi wa wilaya hiyo wanaamini kuwa kurejea kwa watoto hao shuleni ni njia muhimu ya kuwasaidia kutimiza ndoto zao na kuiondoa jamii katika mnyororo wa ujinga na umaskini.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, jumla ya watoto 1,188 wamepata fursa ya kurejeshwa shuleni baada ya kupatiwa vifaa vya masomo kupitia ushirikiano huo na Unicef.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, Damasi Kimaro amesema kati ya watoto hao, wavulana ni 652 na wasichana 536.

Amesisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na kuitaka jamii kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo bila vikwazo.

“Ni wajibu wa jamii nzima, wakiwemo viongozi wa dini, Serikali na wadau wa maendeleo, kuhamasisha watoto kurejea na kuendelea na masomo,” amesema Kimaro.

Amebainisha kuwa katika zoezi hilo, wanafunzi wamekabidhiwa vifaa mbalimbali ikiwemo mabegi ya shule, madaftari, kalamu, penseli pamoja na taulo za kike kwa wanafunzi wa kike.

Jumla ya shule 10 za msingi kutoka kata tano za Wilaya ya Ileje zinazotekeleza mradi wa Educate a Child unaofadhiliwa na Unicef zimenufaika na msaada huo, hatua inayotarajiwa kuongeza motisha ya wanafunzi na kupunguza changamoto za mahudhurio shuleni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *