
Zanzibar. Zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka Chuo Kikuu cha SUMAIT na Karume Institute of Science and Technology wamejitokeza kushiriki futari iliyoandaliwa na Kampuni ya mawasiliano, Yas Tanzania, tukio ambalo ni muendelezo na utamaduni wa Kampuni hiyo kujumuika na jamii katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hafla hiyo ya futari ilifanyika jana katika viwanja vya chuo cha SUMAIT ikiwakutanisha wakufunzi, wanafunzi na timu ya Yas.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni, Mkurugenzi wa Yas – Zanzibar, Ndugu Aziz Said Ali, alisema tukio hilo ni sehemu ya dhamira ya kampuni kujenga ukaribu na jamii kupitia matendo yanayogusa watu moja kwa moja. Alieleza kuwa Ramadhani ni muda wa kutafakari na kujenga undugu, na Yas imekuwa ikitumia kipindi hiki kuungana na watanzania katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Leo tumekuja hapa SUMAIT kushiriki futari na zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka chuoni hapa na chuo cha Karume. Kwetu Yas, hili si tukio la kijamii tu ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii inayotuzunguka. Vijana hawa ndiyo nguvu ya taifa, na tunajivunia sana kuwa karibu nao,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali Watu SUMAIT, Bw. Salum Abdurahman Salum alitoa shukrani kwa Yas na Mixx kwa kuendelea kuwafikia wanafunzi wa Zanzibar kupitia matendo ya upendo na kuonyesha mfano wa namna sekta binafsi inavyoweza kujitoa kwa jamii. Alisema kitendo hicho kina umuhimu mkubwa kwa jamii.
“Kwa niaba ya Chuo cha SUMAIT, niwapongeze Yas na Mixx kwa moyo wa upendo wa kuchukua uamuzi wa kufutarisha wanawafunzi wa chuo chetu na wale wa chuo cha Karume.
Hafla imehitimishwa kwa wanafunzi na wageni kukaa pamoja kufuturu, ikiwa ni alama ya mshikamano na kuenzi maadili ya amani na umoja yanayosisitizwa katika mwezi huu wa ibada.