
Shirika la Amnesty International limetangaza kwamba Marekani lazima iwajibishwe kwa mauaji ya wanafunzi katika Shule ya Msingi ya Minab nchini Iran.
Zaidi ya wanafunzi 160 wa kike na walimu wao wasiopungua 20 waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa kutokana na shambulizi lililofanywa na Marekani na Wazayuni katika Shule ya Shajara Tayyiba katika mji wa Minab kusini mwa Iran katika siku ya kwanza ya vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Sasa shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetangaza kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wa mauaji ya wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Minab, Marekani lazima iwajibishwe kwa uhalifu wake dhidi ya shule hiyo na mauaji ya wanafunzi wa kike.
Shirika hilo limesema Marekani haikuchukua tahadhari zinazofaa za kuzuia madhara ya raia na ilikiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Amnesty International imesisitiza kwamba wale “waliohusika kupanga na kutekeleza shambulio haramu la Marekani dhidi ya shule huko Minab” lazima wawajibishwe.
Shirika hilo la kimataifa limetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi kuhusu uhalifu huo.