Musoma. Watoto 832,448 wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 10 mkoani Mara wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa polio, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuzuia na kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Kampeni hiyo itahusisha mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita, kufuatia kubainika kwa kirusi cha polio katika sampuli za maji machafu mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumanne Machi 17, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu amesema kampeni hiyo itafanyika kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026.

Amesema licha ya uwepo wa kirusi hicho kubainika Mwanza, hadi sasa hakuna mgonjwa wa polio aliyeripotiwa nchini, akibainisha kuwa mara ya mwisho ugonjwa huo kuripotiwa ilikuwa Julai 1996.

“Hatua hii ni ya tahadhari ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu hatari. Serikali imeamua kufanya kampeni ya kitaifa kuimarisha kinga kwa watoto waliolengwa,” amesema Dk Masatu.

Amewataka wakazi wa mkoa huo kushiriki kikamilifu ili kufanikisha zoezi hilo, akisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na polio ni miongoni mwa magonjwa 14 yanayozuilika kwa chanjo.

Ameeleza kuwa polio ni ugonjwa hatari unaosababisha ulemavu wa kudumu na hata kifo, huku akibainisha kuwa hauna tiba, hivyo chanjo ndiyo kinga pekee.

Pia ameitaka jamii kuachana na dhana potofu zinazohusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina, akisisitiza kuwa watoto wote walioko kwenye kundi lengwa wanapaswa kupata chanjo hata kama walishapatiwa hapo awali.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Mara, Flowina Muuzaji amesema zoezi hilo litafanyika kwa mfumo wa nyumba kwa nyumba, pamoja na kufikia shule na vituo vya afya.

“Kila mtoto atakayepata chanjo atawekewa alama maalum ili kuepuka kurudiwa. Maandalizi yanaendelea vizuri, tunachohitaji ni ushirikiano wa jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kushiriki kutoa elimu kwa waumini wao ili kuongeza mwitikio chanya.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wameeleza umuhimu wa kampeni hiyo, wakihimiza jamii kujitokeza ili kuzuia kurejea kwa ugonjwa huo.

“Mimi nilikuwa na jirani mwenye watoto saba, watano walipooza kwa polio kutokana na ukosefu wa elimu na chanjo wakati huo. Sitamani hali ile ijirudie,” amesema Selfina Majura.

Naye Edward Lucas amesema ni muhimu kwa jamii kuelewa athari za polio na kushiriki kikamilifu katika chanjo ili kulinda afya ya watoto na taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *