ARUSHA: Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amewataka wakurugenzi wa bodi na watendaji wakuu wa kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache kuachana na usimamizi wa kawaida na kuelekea kwenye uongozi wa kimkakati unaotazama mbele.
Akizungumza katika Mkutano wa Wakurugenzi wa Kampuni zenye hisa chache za Serikali (MIF 2026) unaofanyika kwa siku tatu jijini Arusha kuanzia Machi 16, 2026, Mchechu alisema mabadiliko hayo ni muhimu ili kampuni ziweze kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia.
Alisema taasisi zinapaswa kujenga utamaduni wa ubunifu, fikra za mbele na maamuzi ya haraka ili kutumia kikamilifu fursa zinazojitokeza na kuongeza mchango katika uchumi wa taifa.
“Katika dunia ya leo inayobadilika kwa kasi kiuchumi na kiteknolojia, uongozi hauwezi tena kujikita kusimamia hali ya sasa pekee, bali unapaswa kutazama mbele na kujiandaa kwa siku za usoni,” alisema.
Mchechu alieleza kuwa jukwaa hilo, linalofanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa mwaka 2024, limeendelea kuwa muhimu katika kuimarisha mjadala kuhusu utawala bora, utendaji na mchango wa kampuni katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Kutoka ufuatiliaji wa kawaida hadi uongozi wa kimkakati unaotazama mbele,” inaakisi msisitizo wa kubadilisha namna ya uongozi ili kuendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi.
Aliongeza kuwa uwekezaji wa Serikali katika kampuni zenye hisa chache umeongezeka kutoka Sh bilioni 821 hadi Sh trilioni 3.6 , huku gawio likiongezeka kutoka Sh bilioni 58 hadi Sh bilioni 266 katika kipindi cha miaka mitano, sawa na ongezeko la asilimia 357.
Alisema mwenendo huo unaonyesha umuhimu wa kuimarisha zaidi uongozi wa kimkakati ili kuongeza thamani ya uwekezaji wa umma na kuchangia malengo ya muda mrefu ya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo 2050.
