Chanzo cha picha, Getty Images
Robert Mueller, mshauri maalum aliyeongoza uchunguzi kuhusu kuingilia kati kwa Urusi katika uchaguzi wa Marekani wa 2016, na ambaye uchunguzi wake ulitikisa sehemu kubwa ya awamu ya kwanza ya utawala wa Donald Trump madarakani, amefariki akiwa na miaka 81.
Sababu ya kifo chake haijajulikana mara moja. CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, imethibitisha kifo chake.
“Kwa huzuni kubwa, tunatoa taarifa kwamba Bob amefariki,” familia yake ilisema katika taarifa kwenda AP Jumatano usiku. “Familia yake inawaomba waheshimu faragha yao.”
Mueller hapo awali aliongoza FBI kuanzia 2001 hadi 2013, akiwa ameteuliwa siku chache kabla ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Ana sifa ya kuibadilisha FBI kuwa shirika la kisasa la kukabiliana na ugaidi.
Uchunguzi wake uligusa kampeni ya Trump mwaka 2016 na kusababisha ukosoaji mkali kutoka kwa rais huyo.
Rais Donald Trump aliandika Jumamosi kwenye mtandao wake: “Ninafurahi amefariki. Huwezi tena kuumiza watu wasio na hatia!”
Waajiri wake wa zamani na wafanyakazi wenzake walimpongeza kama mtumishi wa umma wa muda mrefu.
Marais wote wawili aliowahudumia akiwa mkurugenzi wa FBI – George W. Bush na Barack Obama – walitoa heshima kwa kifo chake.