RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, na kufanya mazungumzo yaliyojikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Zanzibar,Dk.Mwinyi amesema ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani unatarajiwa kuondoa changamoto zilizopo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanyika.


Amesema mradi huo unajumuisha mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 200, matangi ya kuhifadhi mafuta pamoja na bandari yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi. SOMA : Dk. Mwinyi Azindua Uwanja wa Gombani
Aidha, Dk. Mwinyi ameihakikishia Marekani kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuishukuru kwa mchango wake kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar. Amesema bado zipo fursa nyingi kwa makampuni na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza Zanzibar.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Andrew Lentz, amepongeza maendeleo yanayofanyika Zanzibar, hususan katika ujenzi wa miundombinu, akisema ni msingi muhimu katika kuvutia uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi. Pia ameahidi kuwa Marekani itaendelea kupanua ushirikiano na Zanzibar, hususan katika sekta za afya, mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.