
Angalau watu 66 wamefariki na makumi kadhaa wamejeruhiwa wakati ndege ya kijeshi iliyokuwa imebeba watu 125 ilipoanguka wakati wa kupaa kusini mwa Colombia, kulingana na taarifa mpya iliyotolewa kwa shirika la habari la AFP na chanzo cha kijeshi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ndege hiyo, C-130 Hercules, ilianguka yapata saa 4:00 asubuhi (11:00 jioni saa za Ufaransa) muda mfupi baada ya kupaa kutoka Puerto Leguizamo, katika eneo la kusini ya Putumayo, karibu na mpaka na Ecuador, kwa sababu ambazo bado hazijajulikana.
Kulingana na chanzo cha kijeshi, ajali hiyo ilisababisha vifo vya wanajeshi 58, wafanyakazi sita wa jeshi la anga, na maafisa wawili wa polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Anga, Carlos Fernando Silva Rueda, kulikuwa na abiria 114 wengi wanajeshi, na wafanyakazi 11 ndani ya ndege aina ya C-130 Hercules wakati wa ajali hiyo.
Naibu wa meya wa mji huo Carlos Claros amesema karibu watu 81 walijeruhiwa katika mkasa huo. Mji wa Puerto Leguizamo uko Putumayo, jimbo la Amazon linalopakana na Equador na Peru. Waziri wa Ulinzi Pedro Sánchez alisema kwenye mtandao wa X kwamba ndege iliyoanguka Jumatatu ilikuwa ikiwasafirisha wanajeshi hadi mji mwingine huko Putumayo.
Sánchez alisema kuwa hadi sasa hakuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba ndege hiyo ilishambuliwa na makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao karibu na Puerto Leguizamo nchini Colombia. Jeshi la anga lilisema katika taarifa kwamba kiasi ya watu 77 waliokolewa kutoka eneo la ajali wakiwa na majeraha.
Waziri wa Ulinzi, Pedro Sánchez, alisema ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa, ikidondoka takriban kilomita 1.5 kutoka uwanja wa ndege ilikotoka.
Awali, waziri huyo alithibitisha kuwa taratibu zote za kuwasaidia waathiriwa na familia zao zimeanzishwa, pamoja na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
Msemaji kutoka Wizara ya Ulinzi alisema kwamba maafisa bado wanachunguza idadi ya mwisho ya vifo. Vyombo vya habari vilisambaza video za wanajeshi wakiondolewa haraka kutoka eneo hilo kwa pikipiki zilizoendeshwa na wakazi wa eneo hilo, huku kundi lingine la wakaazi likijaribu kuzima moto ambao ndege hiyo ilisababisha katika uwanja uliozungukwa na majani mengi.
Meya wa Puerto Leguízamo, Luis Emilio Bustos, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wasiopungua 34 wamefariki, idadi iliyothibitishwa pia na vyanzo viwili vya kijeshi. Gavana wa mkoa wa Putumayo, Jhon Gabriel Molina, naye alithibitisha idadi hiyo.