Sekta ya madini imeendelea kuonyesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa uchumi nchini baada ya kuchangia asilimia 12.7 ya Pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025.

Hayo yameelezwa leo Machi 24, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, mhandisi, Yahya Samamba akifungua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini kwa mwaka wa Fedha 2025/2026, lililofanyika katika ukumbi wa Midland Hotel, jijini Dodoma.

Mhandisi Samamba amesema thamani ya mauzo ya mazao ya madini nje ya nchi kwa mwaka 2025 imefikia dola za Marekani milioni 4,119 sawa na zaidi ya Sh10.3 trilioni.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini, hususan kupitia uanzishwaji na uboreshaji wa masoko ya madini pamoja na mikakati madhubuti ya kudhibiti utoroshaji wa madini.

Naye mwakilishi wa Afisa Kazi Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmary amesema Ofisi ya Kamishna wa Kazi inajivunia ushirikiano na mafanikio ya Wizara ya Madini katika kuzingatia masuala ya haki na ustawi wa wafanyakazi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa TUGHE Taifa, Happiness Kitarima, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza kwa vitendo misingi na kanuni za chama hicho, ikiwemo kulinda maslahi ya watumishi na kuimarisha mahusiano kazini.

Takwimu hizo zinaashiria kuimarika kwa mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa sambamba na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni na kudhibiti mianya ya upotevu wa rasilimali.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *