SERIKALI imesema imeanza mazungumzo na UNESCO pamoja na Meta Platforms ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inatambuliwa rasmi kwenye majukwaa ya kimtandao, hatua itakayowawezesha watengeneza maudhui kulipwa stahiki kulingana na kazi zao.
Akizungumza katika Kongamano la 5 la Idhaa za Kiswahili Duniani linaloendelea jijini Arusha Machi 24, 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya maudhui ya Kiswahili katika uchumi wa kidijitali.
Amesema licha ya maudhui ya Kiswahili, hasa kutoka Tanzania, kuwa na ubora na kuvutia watazamaji wengi, watengeneza maudhui wamekuwa wakilipwa kiasi kidogo kutokana na lugha hiyo kutotambuliwa rasmi na majukwaa makubwa ya mitandao ya kijamii ikilinganishwa na Kiingereza.
“Unaweza kukuta mtanzania ana wafuasi zaidi ya milioni tatu na maudhui yake yanatazamwa na wengi, lakini hapati mapato kupitia majukwaa kama Facebook, Instagram au TikTok kwa sababu Kiswahili bado hakijatambuliwa rasmi,” alisema Makonda.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo zikifanikiwa, zitafungua fursa mpya za ajira na kuongeza kipato kwa vijana wanaojihusisha na utengenezaji wa maudhui ya kidijitali nchini na barani Afrika kwa ujumla. SOMA: Makonda ataka historia Dar City
