
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China wamezungumza kwa simu na kujadili matukio ya hivi sasa kuhusiana na Vita vya Ramadhani.
Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, wamezungumza kwa simu na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya kikanda na taathira za mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.
Katika mazungumzo hayo, Araqchi ametoa maelezo kuhusu uhalifu na jinai za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kuzitaja kuwa sababu kuu za hali inayoshuhudiwa sasa katika eneo hili na kusisitiza azma thabiti ya Iran ya kuendelea kutetea mamlaka ya kujitawala ya taifa na umoja wa ardhi nzima ya Jamhuri ya Kiislamu hadi hapo malengo yote yatakapotimizwa na adui ajutie kuanzisha uvamizi wake wa kikatili dhidi ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa hali ya mambo katika Mlango-Bahari wa Hormuz haiwezi kutenganishwa na hali jumla ya Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa: “Ukosefu wa usalama uliosababishwa katika Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz ni matokeo ya uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni. Amesema kuwa hatua na mipango inayotekelezwa na Iran ni kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ni katika kulinda mamlaka ya kitaifa na usalama wa Iran ili kuzuia wavamizi kutumia vibaya njia hii ya maji kufanya mashambulizi dhidi ya Iran.”
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa China kwa mara nyingine tena amesisitiza msimamo wa nchi yake wa kulaani mashambulizi haramu ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupinga kukiukwa mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi nzima ya Iran. Wang Yi pia ameashiria uhusiano mzuri kati ya nchi mbili za Iran na China na kusema: Beijing inasisitiza udharura wa kukomeshwa vitendo vya mabavu na uonevu kimataifa na inataka kuheshimiwa diplomasia na sheria za kimataifa ili kutatua mizozo na migogoro mbalimbali.