FAO imekarabati zaidi ya kilomita 300 za mifereji ya umwagiliaji ili kurejesha upatikanaji wa maji katika mashamba na kwa jamii, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha ustahimilivu wa wakazi wa maeneo haya kame nchini Somalia. Wakulima wanasema wameanza kuona matumaini mapya kwani mradi huu wa CLIMB umeboresha maisha yao. 

Nuur Mukhtar Mohamed ni mmoja wao, anasema uhaba wa maji katika Mto Jordan ulikuwa umeathiri vibaya shughuli za kilimo.

Akifafanua anasema, “hapo awali tulikumbana na changamoto kubwa kwa sababu Mto Juba uko chini kuliko mashamba yetu, hali iliyofanya umwagiliaji kuwa mgumu sana. Hata hivyo, mfereji mpya ulioinuliwa umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu.”

Kwa mujibu wa wakulima wengine, maboresho hayo yameleta unafuu mkubwa katika shughuli za kilimo na maisha ya kila siku. 

Akiwa shambani, Sadiyo Sheikh Ali, mkulima kutoka kijiji cha Bulo Bartire, anaeleza kwamba,“Kabla ya mfereji huu, maji yalikuwa haba sana kiasi cha kusababisha migogoro baina ya wakulima. Sasa hali imeimarika na tuna matumaini mapya. Tumeanza kupata utulivu wa akili.”

Mbali na ukarabati wa mifereji, FAO pia inawapatia wakulima mbegu bora na kuwawezesha kuanzisha vikundi vya Akiba na Mikopo vya Kijiji (VSLA), vinavyosaidia kukuza kipato na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Akizungumzia umuhimu wa vikundi hivyo, Yusuf Abdisalam Yusuf, Mkuu wa Kikundi cha Midinimo kutoka Goobweyn, amesema “tumeunda kikundi hiki ili kushirikiana na kusaidiana katika shughuli za kilimo na maisha kwa ujumla, bila kujali ukubwa wa msaada.”

Mifereji iliyokarabatiwa sasa inaendelea kufufua matumaini na kuleta fursa mpya za kipato katika eneo la Jubaland. Hata hivyo, wakulima wanasisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongezewa pembejeo, msaada wa kifedha na mafunzo endelevu ili kuhakikisha jamii zinaendelea kustawi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *