Baadhi ya miili inaonekana kutoka hospitali katika kaunti jirani

Takriban miili 32, mingi yao ikiwa ya watoto wachanga, imefukuliwa kutoka kaburi la pamoja katika mji wa magharibi mwa Kenya, Kericho, huku uchunguzi ukiendelea kuhusu ugunduzi huu wa kushangaza.

Ufukuaji huo ulifanyika baada ya polisi kupata amri ya mahakama ya kufukua miili 14, ambayo awali iliaminika kuzikwa katika eneo hilo.

Mchunguzi wa maiti wa serikali, Richard Njoroge, aliwaambia waandishi wa habari Jumanne jioni kwamba kile walichokigundua kilikuwa “cha ajabu”, huku miili ikiwa “imerundikwa kwenye mifuko ya gunia”, baada ya mchakato wa mchana mzima uliyotatizwa na mvua kubwa.

Uchunguzi wa kina wa maiti ulitarajiwa kuanza leo Jumatano wiki hii, huku kukiwa na wito wa kutambua mara moja miili hiyo ya kuchunguza mazingira ya vifo hivyo.

Njoroge ambaye ni mkaguzi wa maiti wa serikali alisema kulikuwa na watu wazima saba na watoto 25, huku watoto wakiwa wachanga na vijusi. Sehemu kadhaa za miili pia zilipatikana.

Aliongeza kuwa baadhi ya miili ilionekana kutoka hospitali na mochari, jambo litakalothibitishwa zaidi baada ya uchunguzi wa kina. Pia alitaja kuwa miili ya watu wakubwa ilikuwa imeharibika sana, huku ile ya watoto ikiwa haijaharibika kwa kiwango hicho, ikionyesha vifo vilitokea katika nyakati tofauti.

Jumanne, waendesha mashtaka wa mauaji na timu za uchunguzi, wakiwa wamevaa mavazi ya kinga meupe, glovu na barakoa, walifanya kazi chini ya ulinzi mkali huku wakichimba kwenye eneo hilo. Baadhi ya miili ilipatikana kamili, huku mingine ikipatikana sehemu tu na mifupa, ikihifadhiwa katika mifuko ya ushahidi.

Polisi walifunga eneo hilo huku umati wa wakazi ukikusanyika karibu. Wengine walionekana wakiwa wameshikwa na hofu wakati wakaguzi waliporekodi kila hatua ya uchimbaji. Uchimbaji huu ulifanyika kufuatia taarifa kutoka kwa mlalamishi, iliyosababisha polisi kuanzisha uchunguzi.

Siku ya Jumatatu, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema matokeo yao ya awali yanaonyesha kuwa miili 13 isiyodaiwa ilitolewa rasmi kutoka hospitali iliyoko kaunti jirani ya Nyamira na kuhamishwa Kericho kwa mazishi Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, maswali mengi bado yapo kuhusu miili ya ziada na jinsi ilivyozikwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *