Wakati Myanmar inaadhimisha mwaka mmoja tangu tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Machi mwaka jana 2025, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaonya kuwa jamii zinazojaribu kujijenga upya sasa zinakabiliwa na changamoto mpya: athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati kwenye bei za mafuta, chakula na mbolea zinawasukuma familia zilizo hatarini zaidi karibu na njaa.

Ufuatiliaji wa hivi karibuni wa WFP unaonesha kuwa urejeaji baada ya tetemeko hilo bado ni dhaifu. Katika maeneo yaliyoathirika ya Sagaing na Mandalay, kaya moja kati ya sita bado zinakabiliwa na ukosefu wa chakula wa wastani hadi mkali. Nusu ya familia zote bado ziko katika hali ya uhakika wa chakula wa kiwango cha chini na zinaishi siku hadi siku na haziwezi kustahimili hata msukosuko mdogo. Na sasa, msukosuko huo mpya umeanza kuonekana.

“Watu walionusurika tetemeko la ardhi hawajapata hata muda wa kusimama tena, na sasa pigo lingine linawarudisha chini,” anasema Michael Dunford, Mkurugenzi wa WFP nchini Myanmar na kuongeza kuwa , “wimbi hili jipya la misukosuko ya kimataifa linakuja wakati mbaya zaidi kwa Myanmar.”

Hali tete ya Mashariki ya Kati

Mgogoro wa Mashariki ya Kati unavuruga usafirishaji na kusababisha uhaba wa mafuta kote Myanmar. Kupanda kwa bei ya mafuta kunachochea ongezeko la gharama za kusafirisha chakula na bidhaa za kilimo, na kuongeza mzigo kwa familia ambazo tayari zinapata shida kumudu mahitaji ya msingi.

Mgogoro huu pia unawaathiri wakulima wa Myanmar wanapojiandaa kwa msimu wa kilimo wa mvua za masika. Mahitaji ya mbolea yanatarajiwa kuongezeka katika miezi mitatu ijayo, huku uhaba wa mafuta na kupanda kwa gharama za pembejeo vikitarajiwa kuongeza gharama za uzalishaji hadi kufikia mara mbili ya kiwango cha mwaka uliopita.

Mishtuko hii inayoongezeka inatarajiwa kuathiri zaidi maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na tetemeko la ardhi kama vile Chin, Kachin, Kayah, Rakhine, Sagaing na Shan, na kuzidisha ukosefu wa chakula katika nchi ambayo watu milioni 12.4, karibu robo ya idadi ya watu tayari wanakabiliwa na njaa kali.

Jitihada za WFP

Katika mwaka uliopita, WFP ilifikia manusura nusu milioni wa tetemeko hilo kwa msaada wa dharura na uokoaji. Sasa WFP imeanza kuhama kutoka msaada wa dharura kwenda kwenye kurejesha miundombinu ya jamii inayoweza kutoa uthabiti wa muda mrefu.

WFP inahitaji dola za Marekani milioni 150 kwa mwaka 2026 ili kuwasaidia watu milioni 1.5 kote nchini kwa msaada wa kuokoa maisha na kujenga uwezo wa kustahimili majanga. Bila ufadhili wa kutosha, WFP italazimika kuweka kipaumbele kwenye mahitaji ya dharura ya kuokoa maisha, jambo linaloweza kupunguza juhudi za uokoaji zinazosaidia manusura kujenga upya maisha yao na kupunguza utegemezi wa muda mrefu kwa misaada.

“Watu wa Myanmar wamekumbana na misukosuko mfululizo, migogoro, majanga ya tabianchi, tetemeko kubwa la ardhi, na sasa mgogoro wa kimataifa wa mafuta,” anaonya Bwana Dunford na akishauri kwamba, “ni lazima tusimame nao sasa. Mwaka mmoja baada ya tetemeko la ardhi, hawawezi kumudu kuanguka tena.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *