Shule ya Sekondari Kihonda iliyopo Manispaa ya Morogoro, Mkoani Morogoro, imeandika historia mpya baada ya kuibuka kinara wa ufaulu katika shule za kata, kufuatia kupata wastani wa GPA 3.45 kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka 2025.
Mafanikio hayo yameiwezesha shule hiyo kushika nafasi ya kwanza katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, hatua inayodhihirisha juhudi za pamoja za walimu, wanafunzi na wadau wa elimu kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa bendera nyeupe ya ishara ya ushindi pamoja na vyeti vya pongezi kwa walimu, Diwani wa Kata hiyo, Mhandisi Hamis Ndwata, amesema ushindi huo si wa bahati, bali umetokana na kujituma, nidhamu na ubunifu wa walimu katika ufundishaji.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa Manispaa ya Morogoro, Ramadhani Lavaga, ameupongeza uongozi wa shule hiyo na kuwataka kuongeza bidii zaidi ili kudumisha nafasi yao ya uongozi kitaaluma na kuwa mfano kwa shule zingine.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Zaidu Mwaluko, amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati madhubuti waliyojiwekea, ikiwemo kuongeza muda wa masomo, tathmini za mara kwa mara na ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Profesa Vedasto Ndibalema, amesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote wa elimu ndiyo nguzo kuu ya mafanikio hayo, huku akiahidi kuendelea kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.
Mafanikio ya Shule ya Sekondari Kihonda ni kielelezo cha namna juhudi, mshikamano na uongozi bora vinavyoweza kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.
(Feed generated with FetchRSS)