Katika mjadala wa dharura kuhusu “shambulizi la anga dhidi ya Shule ya Wasichana ya Shajareh Tayyebeh huko Minab, nchini Iran, Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limejadili tukio hilo kama ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.”
Mjadala huu wa dharura unafanyika kufuatia tukio hilo lililotajwa kuwa la kutisha lililofanyika siku ya kwanza kabisa ya mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran.
Simulizi ya mama
Tuanze na simulizi ya Mohaddeseh Fallahat, huyu ni mama wa Iran aliyepoteza watoto wake wawili katika shambulizi hilo ambaye anasema “asubuhi ile ilikuwa kama kawaida.” Aliwafunga wanawe gidamu za viatu na kuwavalisha mabegi mgongoni na hakukuwa na dalili yoyote kwamba hiyo ingekuwa mara ya mwisho, kuonana nao.
Anasema “Walipotoka mlangoni, waliniambia, ‘Mama, njoo utuchukue baada ya shule.’ Sentensi hiyo rahisi sasa inajirudia akilini mwangu mara elfu moja, na kila mara moyo wangu unaungua kwa maumivu. Hakuna mama anayewahi kufikiria atampeleka mtoto wake shuleni kwa tabasamu, kisha akumbane na ukimya. Hakuna mama aliyejiandaa kusikia maneno haya: ‘Mtoto wako hatarudi tena.’”
Jengo moja katika eneo la mashariki mwa Tehran likionesha dalili za uharibifu uliosababishwa na mabomu.
Waokoaji
Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva akiwa Tehran kupitia mawasiliano ya satelaiti, Mkuu wa shirika la Msalaba mwekundu na Hilal nyekundu IFRC, Maria Martinez amesema zaidi ya watu 1,900 wameuawa, wakiwemo wanawake na watoto, na takriban watu 20,000 wamejeruhiwa.
Martinez amesimulia masahibu yanayowakuta watoa huduma ya kwanza “Moja ya nyakati za kushtusha na kuvunja moyo ni pale mhudumu wa uokoaji na utafutaji alipogundua miili ya wafamilia yake mwenyewe chini ya vifusi vya jengo lililoshambuliwa.
Katika mji wa Qom, kusini mwa Tehran, mhudumu mwingine aliokoa mwili wa shangazi yake pamoja na mume wake na mtoto wao mdogo.”
Huo ndio uhalisia wanaokumbana nao wahudumu wa kibinadamu, wanaokoa maisha huku wakibeba maumivu makubwa yasiyovumilika ya kupoteza wapendwa wao.
Mjadala wa Baraza la Haki za Binadamu ukifanyika Geneva Uswisi
Kauli ya UN
Tofauti zozote zilizopo kati ya nchi na nchi, sote tunaweza kukubaliana kuwa hazitatatuliwa kwa kuwaua wanafunzi.
Akizungumza katika mjadala huo wa dharura, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa wito kwa mamlaka za kijeshi za Marekani kuchapisha haraka iwezekanavyo matokeo ya uchunguzi wao kuhusu shambulizi hilo.
Türk amesema “Mashambulizi ya mabomu katika Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab yameibua hofu kubwa na maumivu makali. Picha za madarasa yaliyoharibiwa na wazazi waliogubikwa na huzuni zinaonesha wazi ni nani hulipa gharama kubwa zaidi ya vita: raia wasio na uwezo wowote katika maamuzi yaliyopelekea mzozo. Katika tukio hili, inaripotiwa kuwa wanafunzi, walimu, wafanyakazi wa shule, na wapendwa wao 168 wameathirika.
Maafisa waandamizi wa Marekani wamesema shambulizi hilo linafanyiwa uchunguzi. Natoa wito mchakato huo ukamilike haraka iwezekanavyo, na matokeo yake yawekwe wazi kwa umma. Lazima kuwe na haki kwa madhara makubwa yaliyosababishwa.”