Ripoti mpya ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa HRC, kupitia Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Jamhuri ya Kiarabu ya Syria imeweka wazi ukubwa wa ukatili uliolikumba jimbo la Suwayda mwezi Julai, ukisababisha zaidi ya watu 1,700 kuuawa na karibu 200,000 kulazimika kuyahama makazi yao.

Ukitokana na shuhuda 409 za manusura na mashahidi pamoja na ziara za maeneo yaliyoathirika zaidi, wachunguzi wamebaini uharibifu mkubwa hasa katika maeneo ya jamii ya Druze, ambako nyumba, biashara na maeneo ya ibada yalichomwa moto.

Ukatili wa kutisha wahitaji haki ya haraka

“Ukubwa na ukatili wa ghasia na ukiukwaji uliorekodiwa Suwayda unatia huzuni kubwa,” amesema Paulo Sérgio Pinheiro mwenyekiti wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kwa ajili ya Syria , akisisitiza haja ya hatua za haraka.

Ameongeza kuwa “Jitihada zilizopanuliwa za kuhakikisha uwajibikaji kwa wahusika wote, bila kujali upande au cheo, zinahitajika kwa dharura ili kurejesha imani ya jamii zilizoathirika.”

Tume imeonya kuwa bila mifumo madhubuti ya haki na mazungumzo ya kweli, matumaini ya utulivu yataendelea kuwa dhaifu.

media:entermedia_image:5079ec4f-7b97-446d-9424-e8f3b301b7e9

UN Photo/Jean-Marc Ferré

Mwenyekiti wa tume huru ya kimataifa ya uchunguzi kuhusu Syria Paulo Sérgio Pinheiro

Mawimbi matatu ya ghasia yawalenga raia

Wachunguzi wamehitimisha kuwa ghasia hizo zilijitokeza katika mawimbi matatu yaliyokuwa na mlengo wa kibaguzi wa kidini.

Vikosi vya serikali na washirika wao walituhumiwa kufanya mauaji, mateso na kuwakamata kiholela raia wa Druze katika awamu ya kwanza.

Baadaye, makundi ya Druze yalishambulia jamii ya Bedouin, yakisababisha mauaji zaidi, ufurushwaji na uporaji, kabla ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa wapiganaji wa kikabila yaliyoangamiza tena vijiji vya Druze.

Ripoti inaeleza ukiukwaji huo ikiwemo ukatili wa kijinsia unaoweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita na huenda uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Onyo la uhalifu wa kimfumo na kutokuwajibika

“Ukiukwaji mkubwa uliofanywa na vikosi vya serikali na makundi ya Druze unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita,” amesema Fionnuala Ní Aoláin mwakilishi maalum wa kuchagiza na kulinda ahaki za binadamu huku akipambana na ugaidi, akitaka uchunguzi wa haraka, huru na usioegemea upande wowote.

Ameongeza kuwa ushahidi unaashiria uwezekano wa “mashambulizi ya kimfumo dhidi ya raia,” akisisitiza umuhimu wa msaada wa kimataifa katika kuhakikisha uwajibikaji.

Licha ya uchunguzi wa kitaifa na taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya maafisa, maelezo kuhusu uwajibikaji wa viongozi bado ni machache.

media:entermedia_image:67ecd0bf-d5fa-4f59-be13-73edd5f1c9f7

UN Photo/Jean-Marc Ferré

Fionnuala Ní Aoláin mwakilishi maalum wa kuchagiza na kulinda haki za binadamu huku akipambana na ugaidi

Jamii zaharibika, ufurushwaji waendelea

Athari za kibinadamu zimekuwa kubwa, huku jamii nzima zikisambaratika na mshikamano wa kijamii kudhoofika.

Takriban watu 155,000 waliokimbia makazi yao hasa kutoka vijiji vya Druze vilivyoteketezwa bado hawawezi kurejea, wakati jamii nyingi za Bedouin zinaendelea kuishi katika hali ngumu miezi kadhaa baadaye.

“Tunatoa wito kwa pande zote kuongeza juhudi zao kutimiza wajibu wa kisheria, kulinda raia, na kutatua mgogoro,” amesema Monia Ammar, akisisitiza haki ya wakimbizi kurejea na kujenga upya maisha yao.

Jukumu la kimataifa na mvutano unaoongezeka

Ripoti pia inaonyesha mchango wa wahusika wa nje, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kijeshi ya Israel, katika kuzidisha hali ya sintofahamu, pamoja na ongezeko la chochezi za chuki mtandaoni zinazochochewa na taarifa potofu.

Inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia juhudi za kuimarisha utawala wa sheria, maridhiano na kudhibiti kauli za chuki.

Huku Suwayda ikiendelea kugawanyika na mapigano yakiendelea, Tume imeonya kuwa bila hatua madhubuti, mzunguko wa ghasia na kulipizana kisasi utaendelea kuongezeka na kudhoofisha matumaini ya amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *