
Ongezeko la mashambulizi ya roketi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel, yaliyoelezwa na vyombo vya habari vya Israel kama mashambulizi makali zaidi tangu kuanza kwa vita, limeugeuza mkutano wa baraza la mawaziri la Israel kuwa uwanja wa malumbano makali kati ya waziri wa fedha na mkuu wa majeshi ya utawala huo.
Ripoti zinasema kituo cha matangazo cha serikali ya Israel cha Channel 12 kilikiri jana Alkhamisi kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya roketi kutoka Lebanon yalikuwa miongoni mwa mashambulizi makali zaidi yaliyofanywa na Hizbullah tangu kuanza kwa vita.
Wakati huo huo, mkutano wa baraza la mawaziri la Israel umegeuka kuwa vita vya maneno na malumbano kati ya Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich na Mkuu wa Majeshi ya Israel (IDF) Eyal Zamir.
Migogoro hii ndani ya utawala wa kigaidi wa Israel imetokea saa chache baada ya Eyal Zamir kuonya katika mkutano huo huo kwamba ikiwa mgogoro wa nguvu kazi hautatatuliwa, jeshi la Israel litasambaratika kwa ndani.
Siku chache zilizpita Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon iliweka rekodi mpya baada ya kutekeleza operesheni 61 dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku moja.
Wapiganaji shupavu wa Hizbullah nchini Lebanon wametekeleza operesheni 63 katika duru yao ya hivi karibuni ya mapambano dhidi ya adui Muisraeli katika vita vilivyopewa jina la “al‑Asf al‑Ma’koul”, ambapo operesheni 61 kati ya hizo zilitekelezwa siku ya Jumapili pekee.
Harakati ya Hizbullah imetangaza kuwa ni jukumu lake la kisheria na la kimaadili kulinda ardhi na wananchi wa Lebanon, hususan wakati ambapo adui wa Kizayuni ameendelea kutenda ukatili na kuvuka mipaka na mistari myekundu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Hizbullah inalenga tu ngome za kijeshi tofauti na adui wa Mzayuni ambaye anashambulia na kuua raia wa kawaida.