Muda huo ni kuanzia saa 2.30 usiku hadi saa 3.30 usiku, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya siku hiyo iliyopatiwa jina Saa ya Dunia, kwa lugha ya kiingereza Earth Hour.

Kila mtu ashiriki ili tulinde mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika ujumbe wake ametoa wito kwa wananchi duniani kote kuchukua hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, akihimiza ushiriki mpana katika maadhimisho ya hayo kwa mwaka 2026.

Guterres amesema, “Siku ya Saa ya Dunia ilianza kama ishara ndogo lakini sasa imekuwa harakati ya kimataifa inayowaunganisha watu kote ulimwenguni katika kudai hatua za kulinda mazingira.”

“Mwaka huu, tunapoadhimisha miaka 20 ya mafanikio ya Saa ya Dunia, ninawaalika mamilioni ya watu kuzima taa zisizo za lazima kuanzia saa 2:30 usiku hadi saa 3:30 usiku,” amesema.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa tukio hilo halipaswi kubaki kuwa ishara ya kinadharia pekee, bali liwe kichocheo cha mabadiliko halisi.

Ni wakati wa kuchukua hatua za dharura

Ameeleza kuwa dunia inahitaji kwa dharura kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuharakisha mpito wa haki kutoka matumizi ya nishati ya mafuta kisukuku kwenda nishati safi, pamoja na kutoa msaada wa maana kwa jamii zilizo mstari wa mbele zikiathiriwa vibaya na mabadiliko ya tabianchi.

Guterres pia amehimiza wananchi kupaza sauti na kuhamasisha wengine kuchukua hatua, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa katika kujenga mustakabali wa nishati salama na wenye usawa kwa wote.

Maadhimisho ya Saa ya Dunia yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, huku viongozi wakisisitiza kuwa muda wa kuchukua hatua ni sasa.

Kwa Umoja wa Mataifa, jengo la makao yake makuu jijini New York, Marekani litazimwa taa zote kwa muda kwa muda wote wa kipindi hicho cha saa nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *