Dunia inaendelea kukumbushwa kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na ubaguzi wa rangi, changamoto bado zipo na zinahitaji hatua za haraka.

Hayo yamebainishwa na viongozi wa Umoja wa Mataifa pamoja na watetezi wa haki za binadamu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Ubaguzi wa Rangi, yakirejelea tukio la kihistoria la mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1960 nchini Afrika Kusini, ambapo watu 69 waliuawa na polisi wakidai haki zao kwa amani.

Nafasi ya mauaji ya Sharpeville katika harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi

Akizungumza katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Ofisi hiyo James Waweru, amesema tukio la Sharpeville lilifungua macho ya dunia kuhusu ukatili wa mfumo wa ubaguzi wa rangi, na kusisitiza kuwa bado kuna wajibu wa kulinda mafanikio yaliyopatikana.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema dunia inapaswa kuendelea kupambana ili kuhakikisha haki na usawa vinadumishwa kwa wote.

Miaka 60 ya maadhimisho, miaka 25 ya Azimio la Durban

Maadhimisho ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee, yakilingana na miaka 60 tangu kutangazwa kwa siku hiyo na pia yakikumbusha miaka 25 ya Azimio na Mpango wa Utekelezaji wa Durban, ambao ni mfumo muhimu wa kimataifa wa kupambana na ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na aina nyingine za kutovumiliana. Wataalamu wanasema nyaraka hizo zinaendelea kuwa mwongozo muhimu kwa serikali na jamii katika juhudi za kuleta usawa.

Pengo kati ya ahadi na uhalisia: Hakuna nchi inaweza dai haina ubaguzi

Hata hivyo, licha ya hatua zilizopigwa, viongozi wameonya kuhusu pengo kati ya ahadi na hali halisi.

Kamishna Mkuu Türk amesema kuwa ingawa ubaguzi wa wazi kama ule wa zamani umepungua, bado unaendelea kwa njia fiche kupitia mifumo ya kijamii, kiuchumi na kidijitali.

Aidha, Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Nada Al-Nashif, “amesema hakuna nchi inayoweza kudai kuwa haina tatizo la ubaguzi wa rangi, kwani unaathiri nyanja mbalimbali zikiwemo siasa, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.”

Makundi yaliyo hatarini bado yaathirika zaidi

Kwa upande wa jamii zilizo hatarini zaidi kama vile watu wa jamii ya asili, viongozi wao wamesema bado watu hao wanakumbana na ubaguzi unaochanganya rangi, jinsia na kunyimwa haki za ardhi.

Ketty Marcelo ambaye ni kiongozi wanawake wa jamii ya asili kutoka Andes na Amazon na Rais wa zamani wa Chama cha Kitaifa cha watu wa jamii ya asili ya Andes na Amazon nchini Peru amesema kuwa kuna ahadi nyingi za kimataifa bado hazijatekelezwa kwa vitendo kwa watu wanaokumbwa moja kwa moja na ubaguzi huo.

Naye Beatriz Carrillo de los Reyes, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usawa na Kupinga Ubaguzi kwenye Wizara ya Usawa nchini Hispania ameonya kuwa ubaguzi wa rangi umebadilika na sasa unaonekana hata katika jamii zilizodhaniwa kuwa zimepiga hatua.

Changamoto mpya katika enzi ya kidijitali

Viongozi pia wameeleza kuwa majukwaa ya kidijitali yameongeza changamoto mpya, ikiwemo kuenea kwa kauli zenye chuki na taarifa potofu.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Mabunge Duniani, (IPU) Martin Chungong, amesema wabunge wengi hukumbana na vitisho, hasa kupitia mtandao, hali inayodhoofisha demokrasia na mshikamano wa kijamii.

Wito mkubwa umetolewa wa kufanya mabadiliko ya kimuundo, ikiwemo kuhakikisha uwakilishi wa makundi yote katika maamuzi, kuimarisha haki ya marekebisho kwa waathirika wa ubaguzi wa rangi, na kubadilisha mitazamo inayochochea ubaguzi.

Balozi Waweru amesisitiza kuwa haki ya marekebisho inapaswa kujumuisha kutambua makosa ya kihistoria, kuomba msamaha na kurejesha mali za kitamaduni.

Mapambano ya pamoja yaendelea

Kwa ujumla, viongozi wamekiri kuwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi si jukumu la serikali pekee bali ni la jamii nzima.

Wamehimiza mshikamano wa kimataifa na hatua za pamoja ili kuhakikisha kuwa haki, usawa na heshima vinapatikana kwa wote bila ubaguzi wowote.

Kwa kuhitimisha, Bwana Türk ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kukemea na kuchukua hatua dhidi ya ubaguzi wa rangi kila unapojitokeza, akisisitiza kuwa mapambano haya ni endelevu na yanahitaji ujasiri wa pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *